Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 31:1-13

Kumbukumbu 31:1-13 NENO

Kisha Musa akaenda akasema maneno haya kwa Waisraeli wote: “Sasa nina miaka mia moja na ishirini nami siwezi tena kuwaongoza. Mwenyezi Mungu ameniambia, ‘Hutavuka Yordani.’ Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, yeye mwenyewe atavuka mbele yenu. Ataangamiza mataifa haya mbele yenu, nanyi mtaimiliki nchi yao. Pia Yoshua atavuka mbele yenu, kama Mwenyezi Mungu alivyosema. Naye Mwenyezi Mungu atawafanyia watu hao kile alichowafanyia Sihoni na Ogu, wafalme wa Waamori, ambao aliwaangamiza pamoja na nchi yao. Mwenyezi Mungu atawakabidhi kwenu, nanyi lazima mkawatendee yale yote niliyowaamuru. Kuweni imara na moyo wa ushujaa. Msiogope wala msifadhaike kwa sababu yao, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anaenda pamoja nanyi; kamwe hatawaacha wala hatawatupa ninyi.” Kisha Musa akamwita Yoshua na akamwambia mbele ya Israeli wote, “Uwe imara na moyo wa ushujaa, kwa kuwa ni lazima uende na watu hawa katika nchi ile Mwenyezi Mungu aliyowaapia baba zao kuwapa, nawe ni lazima uwagawie kama urithi wao. Mwenyezi Mungu mwenyewe atakutangulia naye atakuwa pamoja nawe; kamwe hatakuacha wala hatakutupa. Usiogope, wala usifadhaike.” Kwa hiyo Musa akaandika sheria hii na kuwapa makuhani, wana wa Lawi, waliochukua Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu na wazee wote wa Israeli. Kisha Musa akawaamuru, akasema: “Mwishoni mwa kila miaka saba, katika mwaka wa kufuta madeni, wakati wa Sikukuu ya Vibanda, Waisraeli wote wanapokuja mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mahali atakapopachagua, utasoma sheria hii mbele yao masikioni mwao. Kusanya watu wote, wanaume, wanawake, watoto na wageni wanaoishi katika miji yenu, ili waweze kusikia na kujifunza kumcha Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kuzingatia maneno yote ya sheria hii. Watoto wao, ambao hawaijui sheria hii, lazima waisikie na kujifunza kumcha Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa muda mtakaoishi katika nchi mnayovuka Yordani kuimiliki.”