Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 32:15-27

Kumbukumbu 32:15-27 NEN

Yeshuruni alinenepa na kupiga teke; alikuwa na chakula tele, akawa mzito na akapendeza sana. Akamwacha Mungu aliyemuumba, na kumkataa Mwamba Mwokozi wake. Wakamfanya Mungu kuwa na wivu kwa miungu yao migeni, na kumkasirisha kwa sanamu zao za machukizo. Wakatoa dhabihu kwa pepo, ambao si Mungu: miungu wasiyoijua, miungu iliyojitokeza siku za karibuni, miungu ambayo baba zenu hawakuiogopa. Mkamwacha Mwamba, aliyewazaa ninyi; mkamsahau Mungu aliyewazaa. BWANA akaona hili, akawakataa, kwa sababu alikasirishwa na wanawe na binti zake. Akasema, “Nitawaficha uso wangu, nami nione mwisho wao utakuwa nini, kwa kuwa wao ni kizazi kilichopotoka, watoto ambao si waaminifu. Wamenifanya niwe na wivu kwa kile ambacho si mungu, na kunikasirisha kwa sanamu zao zisizokuwa na thamani. Nitawafanya wawaonee wivu wale ambao si taifa. Nitawafanya wakasirishwe na taifa lile lisilo na ufahamu. Kwa maana moto umewashwa kwa hasira yangu, ule uwakao hadi kwenye vina vya mauti. Utateketeza dunia pamoja na mazao yake, na kuwasha moto katika misingi ya milima. “Nitalundika majanga juu yao na kutumia mishale yangu dhidi yao. Nitatuma njaa kali dhidi yao maradhi mabaya, yateketezayo na tauni ya kufisha; nitawapelekea meno makali ya wanyama mwitu, na sumu ya nyoka wale watambaao mavumbini. Barabarani upanga utawakosesha watoto; nyumbani mwao hofu itatawala. Vijana wao wa kiume na wa kike wataangamia, pia watoto wachanga na wazee wenye mvi. Nilisema ningewatawanya na kufuta kumbukumbu lao katika mwanadamu. Lakini nilihofia dhihaka za adui, adui asije akashindwa kuelewa, na kusema, ‘Mikono yetu imeshinda; BWANA hakufanya yote haya.’ ”