Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu la Sheria 32:15-27

Kumbukumbu la Sheria 32:15-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Lakini Yeshuruni alinenepa, akapiga teke; Umenenepa, umekuwa mnene, umewanda; Ndipo akamwacha Mungu aliyemfanya, Akamdharau Mwamba wa wokovu wake. Wakamtia wivu kwa miungu migeni, Wakamkasirisha kwa machukizo. Walitoa sadaka kwa pepo, si Mungu, Kwa miungu wasiyoijua, Kwa miungu mipya iliyotokea siku zilizo karibu, Ambayo baba zenu hawakuiogopa. Humkumbuki Mwamba aliyekuzaa, Mungu aliyekuzaa umemsahau. BWANA akaona, akawachukia, Kwa sababu ya kukasirishwa na wanawe na binti zake. Akasema, Nitawaficha uso wangu, Nitaona mwisho wao utakuwaje; Maana, ni kizazi cha ukaidi mwingi, Watoto wasio imani ndani yao. Wamenitia wivu kwa kisicho Mungu; Wamenikasirisha kwa ubatili wao; Nami nitawatia wivu kwa wasio watu, Nami nitawakasirisha kwa taifa lipumbaalo. Maana, moto umewashwa kwa hasira yangu, Unateketea hata chini ya kuzimu, Unakula dunia pamoja na mazao yake, Unaunguza misingi ya milima. Nitaweka madhara juu yao chunguchungu; Nitawapiga kwa mishale yangu hata ikaishe; Watakonda kwa njaa, wataliwa na makaa ya moto, Na uharibifu mkali; Nitawapelekea meno ya wanyama wakali, Pamoja na sumu ya wadudu watambaao mavumbini. Nje upanga utawafifiliza Na ndani ya vyumba, utisho; Utaangamiza mvulana na msichana, Anyonyaye pamoja na mwenye mvi, Nalisema, Ningewatawanyia mbali, Ningekomesha kumbukumbu lao kati ya wanadamu; Isipokuwa naliogopa makamio ya adui, Adui zao wasije wakafikiri uongo, Wasije wakasema, Mkono wetu umetukuka, Wala BWANA hakuyafanya haya yote.

Kumbukumbu la Sheria 32:15-27 Biblia Habari Njema (BHN)

Watu wa Israeli walinona na kupiga mateke; walinenepa, wakawa na kitambi na kunawiri; kisha wakamwacha Mungu aliyewaumba, wakamdharau Mwamba wa wokovu wao. Walimfanya aone wivu mkali kwa miungu yao, walimchochea akasirike kwa matendo yao ya kuchukiza. Walitambikia majini ambayo hayakuwa miungu, waliiendea miungu ambayo hawakuijua kamwe, miungu mipya iliyotokea siku za karibuni, ambayo wazee wao hawakuiheshimu kamwe. Hamkumjali Mwamba aliyewapa uhai, mlimsahau Mungu aliyewazaa nyinyi. Mwenyezi-Mungu aliona jambo hilo akawaacha; aliwakataa watoto wake, waume kwa wake. Akasema, ‘Nitawaficha uso wangu nione mwisho wao utakuwaje! Maana wao ni kizazi kipotovu, watoto wasio na uaminifu wowote. Wamenichochea kuona wivu kwa kitu kisicho mungu, wamenikasirisha kwa sanamu zao. Hivyo nitawafanya waone wivu kwa kisicho watu, nitawakasirisha kwa kutumia taifa la wapumbavu. Hasira yangu imewaka moto, inachoma mpaka chini kuzimu, itateketeza dunia na vilivyomo, itaunguza misingi ya milima. Nitarundika maafa chungu nzima juu yao, nitawamalizia mishale yangu. Watakonda kwa njaa, wataangamizwa kwa homa kali. Nitapeleka wanyama wenye meno makali kuwashambulia, na nyoka wenye sumu wanaotambaa mavumbini. Vita vitasababisha vifo vingi nje na majumbani hofu itawatawala, vijana wa kiume na wa kike watauawa hata wanyonyao na wazee wenye mvi. Nilisema, ningaliwaangamiza kabisa na kuwafanya wasikumbukwe tena na mtu yeyote, ila tu kwa sababu ya majivuno ya maadui zao ili maadui zao wasije wakafikiria vingine; wasije wakasema, wamefaulu kuwaangamiza, nami Mwenyezi-Mungu sihusiki katika mambo haya!’

Kumbukumbu la Sheria 32:15-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Lakini Yeshuruni alinenepa, akapiga teke; Umenenepa, umekuwa mnene, umewanda; Ndipo akamwacha Mungu aliyemfanya, Akamdharau Mwamba wa wokovu wake. Wakamtia wivu kwa miungu migeni, Wakamkasirisha kwa machukizo. Walitoa sadaka kwa pepo, si Mungu, Kwa miungu wasiyoijua, Kwa miungu mipya iliyotokea siku zilizo karibu, Ambayo baba zenu hawakuiogopa. Humkumbuki Mwamba aliyekuzaa, Mungu aliyekuzaa umemsahau. BWANA akaona, akawachukia, Kwa sababu ya kukasirishwa na wanawe na binti zake. Akasema, Nitawaficha uso wangu, Nitaona mwisho wao utakuwaje; Maana, ni kizazi cha ukaidi mwingi, Watoto wasio imani ndani yao. Wamenitia wivu kwa kisicho Mungu; Wamenikasirisha kwa ubatili wao; Nami nitawatia wivu kwa wasio watu, Nami nitawakasirisha kwa taifa lipumbaalo. Maana, moto umewashwa kwa hasira yangu, Unateketea hata chini ya kuzimu, Unakula dunia pamoja na mazao yake, Unaunguza misingi ya milima. Nitaweka madhara juu yao chungu chungu; Nitawapiga kwa mishale yangu hata ikaishe; Watakonda kwa njaa, wataliwa na makaa ya moto, Na uharibifu mkali; Nitawapelekea meno ya wanyama wakali, Pamoja na sumu ya wadudu watambaao mavumbini. Nje upanga utawafifiliza Na ndani ya vyumba, utisho; Utaangamiza mvulana na msichana, Anyonyaye pamoja na mwenye mvi, Nilisema, Ningewatawanyia mbali, Ningekomesha kumbukumbu lao kati ya wanadamu; Isipokuwa niliogopa makamio ya adui, Adui zao wasije wakafikiri uongo, Wasije wakasema, Mkono wetu umetukuka, Wala BWANA hakuyafanya haya yote.

Kumbukumbu la Sheria 32:15-27 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Yeshuruni alinenepa na kupiga teke; alikuwa na chakula tele, akawa mzito na akapendeza sana. Akamwacha Mungu aliyemuumba, na kumkataa Mwamba Mwokozi wake. Wakamfanya Mungu kuwa na wivu kwa miungu yao migeni, na kumkasirisha kwa sanamu zao za machukizo. Wakatoa dhabihu kwa pepo, ambao si Mungu: miungu wasiyoijua, miungu iliyojitokeza siku za karibuni, miungu ambayo baba zenu hawakuiogopa. Mkamwacha Mwamba, aliyewazaa ninyi; mkamsahau Mungu aliyewazaa. BWANA akaona hili, akawakataa, kwa sababu alikasirishwa na wanawe na binti zake. Akasema, “Nitawaficha uso wangu, nami nione mwisho wao utakuwa nini, kwa kuwa wao ni kizazi kilichopotoka, watoto ambao si waaminifu. Wamenifanya niwe na wivu kwa kile ambacho si mungu, na kunikasirisha kwa sanamu zao zisizokuwa na thamani. Nitawafanya wawaonee wivu wale ambao si taifa. Nitawafanya wakasirishwe na taifa lile lisilo na ufahamu. Kwa maana moto umewashwa kwa hasira yangu, ule uwakao hadi kwenye vina vya mauti. Utateketeza dunia pamoja na mazao yake, na kuwasha moto katika misingi ya milima. “Nitalundika majanga juu yao na kutumia mishale yangu dhidi yao. Nitatuma njaa kali dhidi yao maradhi mabaya, yateketezayo na tauni ya kufisha; nitawapelekea meno makali ya wanyama mwitu, na sumu ya nyoka wale watambaao mavumbini. Barabarani upanga utawakosesha watoto; nyumbani mwao hofu itatawala. Vijana wao wa kiume na wa kike wataangamia, pia watoto wachanga na wazee wenye mvi. Nilisema ningewatawanya na kufuta kumbukumbu lao katika mwanadamu. Lakini nilihofia dhihaka za adui, adui asije akashindwa kuelewa, na kusema, ‘Mikono yetu imeshinda; BWANA hakufanya yote haya.’ ”