Waefeso 6:10-18
Waefeso 6:10-18 NENO
Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana Isa na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kuzipinga hila za ibilisi. Kwa maana kushindana kwetu si dhidi ya mwili na damu, bali dhidi ya falme na mamlaka, dhidi ya wakuu wa ulimwengu huu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja, nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara. Kwa hiyo simameni imara mkiwa mmejifunga kweli kiunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani, nayo miguu yenu ivalishwe viatu vya utayari tunaopata katika Injili ya amani. Zaidi ya haya yote, twaeni ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Vaeni chapeo ya wokovu na mchukue upanga wa Roho wa Mungu, ambao ni neno la Mungu, mkiomba kwa Roho siku zote katika sala zote na maombi, mkikesha kila wakati mkiwaombea watakatifu wote.