Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Esta 9:17-32

Esta 9:17-32 NENO

Hili lilitendeka siku ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari na siku ya kumi na nne walipumzika na kuifanya siku ya karamu na furaha. Wayahudi huko Shushani, hata hivyo, walikuwa wamekusanyika siku ya kumi na tatu na ya kumi na nne, pia siku ya kumi na tano walipumzika na kuifanya siku ya karamu na furaha. Ndiyo sababu Wayahudi wanaokaa vijijini na katika miji midogo huadhimisha siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari kama siku ya furaha na karamu, siku ambayo wao hupeana zawadi mmoja kwa mwingine. Mordekai aliandika matukio haya, naye akapeleka barua kwa Wayahudi wote walio katika majimbo ya Mfalme Ahasuero, majimbo yaliyo mbali na karibu, akiwataka kila mwaka washerehekee siku ya kumi na nne na ya kumi na tano ya mwezi wa Adari kama wakati ambao Wayahudi walipata nafuu kutoka kwa adui zao na kama mwezi ambao huzuni yao iligeuzwa kuwa furaha na kuomboleza kwao kuwa siku ya kusherehekea. Aliwaandikia kushika siku hizo kama siku za karamu na za furaha na kupeana zawadi za vyakula wao kwa wao na zawadi kwa maskini. Hivyo Wayahudi walikubali kuendeleza sherehe walizokuwa wamezianza, wakifanya lile Mordekai alilokuwa amewaandikia. Kwa maana Hamani mwana wa Hamedatha Mwagagi, adui wa Wayahudi wote, alikuwa amepanga hila dhidi ya Wayahudi ili kuwaangamiza, na alikuwa amepiga puri (yaani kura) kwa ajili ya maangamizi na uharibifu wao. Lakini wakati shauri hilo baya lilipoarifiwa kwa mfalme, alitoa amri iliyoandikwa kwamba mipango mibaya ambayo Hamani ameipanga dhidi ya Wayahudi inapasa imrudie juu ya kichwa chake mwenyewe, na kwamba yeye na wanawe waangikwe mahali pa kunyongea watu. (Kwa hiyo siku hizi ziliitwa Purimu, kutokana na neno puri.) Kwa sababu ya kila kitu kilichoandikwa kwenye barua hii na kwa sababu ya yale waliyoyaona na yale yaliyowatokea, Wayahudi wakachukua na kuimarisha desturi kwamba wao na wazao wao na wote ambao walijiunga nao wangezishika siku hizi mbili kila mwaka bila kuacha, kwa njia ilivyoelekezwa na kwa wakati wake. Siku hizi zinapasa zikumbukwe na kuadhimishwa katika kila kizazi, kila jamaa na katika kila jimbo na kila jiji. Nazo siku hizi za Purimu kamwe zisikome kusherehekewa na Wayahudi, wala kumbukumbu zake zisipotee miongoni mwa wazao wake. Basi Malkia Esta binti Abihaili, pamoja na Mordekai Myahudi, waliandika kwa mamlaka yote kuthibitisha barua hii ya pili kuhusu Purimu. Naye Mordekai akatuma barua kwa Wayahudi wote katika majimbo mia moja na ishirini na saba (127) ya ufalme wa Ahasuero, barua zenye maneno ya amani na matumaini, ili kuimarisha siku hizi za Purimu katika majira yake yaliyowekwa, kama Mordekai Myahudi na Malkia Esta walivyowaamuru, na walivyojiimarisha wenyewe na wazao wao kuhusu nyakati za kufunga na kuomboleza. Amri ya Esta ilithibitisha taratibu hizi kuhusu Purimu, nayo ikaandikwa katika kumbukumbu.