Kutoka 13:17-22
Kutoka 13:17-22 NEN
Farao alipowaachia watu waende, Mungu hakuwaongoza kufuata njia ipitiayo katika nchi ya Wafilisti, ingawa njia hiyo ilikuwa fupi zaidi. Kwa maana Mungu alisema, “Wakikabiliana na vita, wanaweza kubadili mawazo yao na kurudi Misri.” Kwa hiyo Mungu akawaongoza watu kupitia njia ya kuzunguka kupitia jangwani, kuelekea Bahari ya Shamu. Waisraeli walipanda kutoka nchi ya Misri wakiwa wamejiandaa kwa vita. Mose akachukua mifupa ya Yosefu kwa sababu Yosefu alikuwa amewaapisha wana wa Israeli. Alikuwa amewaambia, “Hakika Mungu atakuja kuwasaidia, nanyi ni lazima mwiichukue mifupa yangu mwende nayo kutoka mahali hapa.” Baada ya Waisraeli kuondoka Sukothi wakapiga kambi huko Ethamu pembeni mwa jangwa. Wakati wa mchana BWANA aliwatangulia kwa nguzo ya wingu kuwaongoza katika njia yao, na wakati wa usiku aliwatangulia kwa nguzo ya moto kuwaangazia, ili waweze kusafiri mchana au usiku. Ile nguzo ya wingu wakati wa mchana au ile nguzo ya moto wakati wa usiku haikuondoka mahali pake mbele ya watu.