Kutoka 2:1-10
Kutoka 2:1-10 NEN
Basi mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaoa mwanamke Mlawi, naye mwanamke huyo akapata mimba, akazaa mtoto wa kiume. Alipoona mtoto huyo ni mzuri, akamficha kwa miezi mitatu. Lakini alipoona hawezi kumficha zaidi, akamtengenezea kisafina cha mafunjo, akakipaka lami. Kisha akamweka huyo mtoto ndani yake, akakificha katikati ya matete kando ya ukingo wa Mto Naili. Dada ya huyo mtoto akasimama mbali ili kuona kitakachompata mtoto. Ndipo binti Farao akateremka mtoni Naili kuoga, nao wahudumu wake wakawa wanatembea ukingoni mwa mto. Binti mfalme akaona kisafina katikati ya manyasi, akamtuma mmoja wa watumwa wake wa kike kukichukua. Alifungua kisafina akaona mtoto ndani yake. Mtoto alikuwa akilia, akamhurumia. Akasema, “Huyu ni mmoja wa watoto wa Kiebrania.” Ndipo dada wa huyo mtoto akamuuliza binti Farao, “Je, niende nikakutafutie mmoja wa wanawake wa Kiebrania akulelee huyu mtoto?” Binti Farao akamjibu, “Ndiyo, nenda.” Yule msichana akaenda akamleta mama wa mtoto. Binti Farao akamwambia, “Mchukue huyu mtoto unisaidie kumlea, nami nitakulipa.” Basi yule mwanamke akamchukua mtoto na kumlea. Mtoto alipokua, akampeleka kwa binti Farao, naye akawa mwanawe. Akamwita jina lake Mose akisema, “Nilimtoa kwenye maji.”