Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kut 2:1-10

Kut 2:1-10 SUV

Mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaondoka akaoa binti mmoja wa Lawi. Yule mwanamke akachukua mimba akazaa mwana, na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu. Na alipokuwa hawezi kumficha tena, akampatia kisafina cha manyasi akakipaka sifa na lami, akamtia mtoto ndani yake, akakiweka katika majani kando ya mto. Umbu lake mtoto akasimama mbali ili ajue yatakayompata. Basi binti Farao akashuka, aoge mtoni, na vijakazi wake wakatembea kando ya mto; naye akakiona kile kisafina katika majani, akamtuma kijakazi wake kwenda kukileta. Akakifungua, akamwona mtoto, na tazama, mtoto yule analia. Basi akamhurumia, akasema, Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania. Basi umbu lake mtoto akamwambia binti Farao, Je! Niende nikamwite mlezi katika wanawake wa Kiebrania, aje kwako, akunyonyeshee mtoto huyu? Binti Farao akamwambia, Haya! Enenda. Yule kijana akaenda akamwita mama yake yule mtoto. Binti Farao akamwambia, Mchukue mtoto huyu, ukaninyonyeshee, nami nitakupa mshahara wako. Yule mwanamke akamtwaa mtoto, akamnyonyesha. Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe. Akamwita jina lake Musa, akasema, Ni kwa sababu nalimtoa majini.