Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 22:7-20

Kutoka 22:7-20 NEN

“Kama mtu akimpa jirani yake fedha au mali nyingine amtunzie, na kama vikiibwa kutoka nyumba ya huyo jirani, kama mwizi atashikwa, lazima alipe mara mbili. Lakini mwizi asipopatikana, mwenye nyumba atafika mbele ya waamuzi ili kuthibitisha kuwa hakuchukua mali ya mwenzake. Pakiwepo jambo lolote la mali isiyo halali, ikiwa ni maksai, punda, kondoo, mavazi, ama mali yoyote iliyopotea ambayo fulani atasema, ‘Hii ni mali yangu,’ pande zote mbili wataleta mashauri yao mbele ya waamuzi. Yule ambaye waamuzi watamwona kuwa na hatia atamlipa jirani yake mara mbili. “Kama mtu akimpa jirani yake punda, ngʼombe, kondoo au mnyama mwingine yeyote amtunzie, akifa au akijeruhiwa au akichukuliwa wakati haonekani na mtu yeyote, jambo hili kati yao wawili litaamuliwa kwa kuapa kiapo mbele za BWANA, kwamba huyo jirani hakuhusika na wizi wa mali ya jirani yake. Mwenye mali itampasa akubali jambo hili, na hakuna malipo yatakayohitajika. Lakini kama mnyama aliibwa kwa jirani, itampasa amlipe mwenye mnyama. Kama ameraruliwa na mnyama pori, ataleta mabaki ya mnyama kama ushahidi, naye hatadaiwa kulipa mnyama aliyeraruliwa. “Kama mtu akimwazima mnyama kutoka kwa jirani yake, na kama akiumia au akafa na mwenye mnyama hayupo, lazima amlipe huyo mnyama. Lakini mwenye mnyama akiwa angalipo na mnyama wake, mwazimaji hatalazimika kumlipa. Kama mnyama alikuwa amekodishwa, fedha iliyolipwa kwa kukodisha inatosha kwa kufidia hasara. “Kama mtu akimshawishi bikira ambaye hajaposwa na akilala naye, lazima alipe mahari, kisha atamwoa msichana huyo. Baba wa msichana akikataa katakata kumpa huyo mtu huyo msichana wake, bado ni lazima huyo mtu atalipa mahari kama inavyostahili malipo ya ubikira. “Usiruhusu mwanamke mchawi aishi. “Mtu yeyote aziniye na mnyama lazima auawe. “Mtu awaye yote anayemtolea mungu mwingine dhabihu isipokuwa BWANA, lazima aangamizwe.