Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 22:7-20

Kutoka 22:7-20 NENO

“Mtu akimpa jirani yake fedha au mali nyingine amtunzie, vitu vile vikiibwa kutoka nyumba ya huyo jirani, kama mwizi akishikwa, lazima alipe mara mbili. Lakini mwizi asipopatikana, mwenye nyumba atafika mbele ya waamuzi ili kuthibitisha kuwa hakuchukua mali ya mwenzake. Pakiwepo jambo lolote la mali isiyo halali, iwe ni maksai, punda, kondoo, mavazi, ama mali yoyote iliyopotea, ambayo mtu fulani atasema, ‘Hii ni mali yangu,’ kila upande utaleta shauri lake mbele ya waamuzi. Yule ambaye waamuzi watathibitisha kuwa ana hatia atamlipa jirani yake mara mbili. “Mtu akimpa jirani yake punda, ng’ombe, kondoo au mnyama mwingine yeyote amtunzie, yule mnyama akifa, au akijeruhiwa, au akiibiwa bila mtu kuona, jambo hili kati yao wawili litaamuliwa kwa kuapa mbele za Mwenyezi Mungu, kwamba huyo jirani hakuhusika na wizi wa mali ya jirani yake. Mwenye mali itampasa akubali jambo hili, na hakuna malipo yatakayohitajika. Lakini kama mnyama aliibwa kwa jirani, itampasa amlipe mwenye mnyama. Kama ameraruliwa na mnyama pori, ataleta mabaki ya mnyama kama ushahidi, naye hatadaiwa mnyama aliyeraruliwa. “Mtu akiazima mnyama kutoka kwa jirani yake, huyo mnyama akiumia au akafa na mwenye mnyama hayupo, lazima amlipe huyo mnyama. Lakini mwenye mnyama akiwa bado ako na mnyama wake, aliyeazima hatalazimika kumlipa. Kama mnyama alikuwa amekodishwa, fedha iliyolipwa kwa kukodisha inatosha kwa kufidia hasara. “Mtu akimshawishi bikira ambaye hajaposwa na akalala naye, lazima alipe mahari, kisha atamwoa msichana huyo. Baba wa msichana akikataa katakata kumpa huyo mtu binti yake, bado ni lazima huyo mtu atalipa mahari kama inavyostahili malipo ya ubikira. “Usiruhusu mwanamke mchawi aishi. “Mtu yeyote aziniye na mnyama lazima auawe. “Mtu yeyote anayemtolea mungu mwingine dhabihu isipokuwa Mwenyezi Mungu, lazima aangamizwe.