Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 22

22
Ulinzi wa mali
1“Mtu yeyote akiiba maksai au kondoo na kumchinja au kumuuza, ni lazima alipe ng’ombe watano badala ya maksai mmoja na kondoo wanne badala ya kondoo mmoja.
2“Mwizi akishikwa akivunja nyumba akapigwa hata akafa, aliyemuua hana hatia ya kumwaga damu; 3lakini jambo hilo likitokea wakati jua limechomoza, huyo mtu atakuwa na hatia ya kumwaga damu.
“Mwizi huyo sharti alipe, lakini kama hana kitu, lazima auzwe ili alipe kwa ajili ya wizi wake.
4“Mnyama aliyeibwa akikutwa hai mkononi mwake, iwe ni maksai au punda au kondoo, lazima alipe mara mbili.
5“Mtu akichunga mifugo yake katika shamba au shamba la mizabibu, na akawaachia walishe katika shamba la mtu mwingine, ni lazima alipe vitu bora kutoka shamba lake mwenyewe au kutoka shamba lake la mizabibu.
6“Moto ukiwaka na kuenea kwenye vichaka vya miiba na kuteketeza miganda ya nafaka au nafaka ambayo haijavunwa, au kuteketeza shamba lote, mtu yule aliyewasha moto lazima alipe.
7“Mtu akimpa jirani yake fedha au mali nyingine amtunzie, vitu vile vikiibwa kutoka nyumba ya huyo jirani, kama mwizi akishikwa, lazima alipe mara mbili. 8Lakini mwizi asipopatikana, mwenye nyumba atafika mbele ya waamuzi ili kuthibitisha kuwa hakuchukua mali ya mwenzake. 9Pakiwepo jambo lolote la mali isiyo halali, iwe ni maksai, punda, kondoo, mavazi, ama mali yoyote iliyopotea, ambayo mtu fulani atasema, ‘Hii ni mali yangu,’ kila upande utaleta shauri lake mbele ya waamuzi. Yule ambaye waamuzi watathibitisha kuwa ana hatia atamlipa jirani yake mara mbili.
10“Mtu akimpa jirani yake punda, ng’ombe, kondoo au mnyama mwingine yeyote amtunzie, yule mnyama akifa, au akijeruhiwa, au akiibiwa bila mtu kuona, 11jambo hili kati yao wawili litaamuliwa kwa kuapa mbele za Mwenyezi Mungu, kwamba huyo jirani hakuhusika na wizi wa mali ya jirani yake. Mwenye mali itampasa akubali jambo hili, na hakuna malipo yatakayohitajika. 12Lakini kama mnyama aliibwa kwa jirani, itampasa amlipe mwenye mnyama. 13Kama ameraruliwa na mnyama pori, ataleta mabaki ya mnyama kama ushahidi, naye hatadaiwa mnyama aliyeraruliwa.
14“Mtu akiazima mnyama kutoka kwa jirani yake, huyo mnyama akiumia au akafa na mwenye mnyama hayupo, lazima amlipe huyo mnyama. 15Lakini mwenye mnyama akiwa bado ako na mnyama wake, aliyeazima hatalazimika kumlipa. Kama mnyama alikuwa amekodishwa, fedha iliyolipwa kwa kukodisha inatosha kwa kufidia hasara.
Uwajibikaji wa kijamii
16“Mtu akimshawishi bikira ambaye hajaposwa na akalala naye, lazima alipe mahari, kisha atamwoa msichana huyo. 17Baba wa msichana akikataa katakata kumpa huyo mtu binti yake, bado ni lazima huyo mtu atalipa mahari kama inavyostahili malipo ya ubikira.
18“Usiruhusu mwanamke mchawi aishi.
19“Mtu yeyote aziniye na mnyama lazima auawe.
20“Mtu yeyote anayemtolea mungu mwingine dhabihu isipokuwa Mwenyezi Mungu, lazima aangamizwe.
21“Usimtendee mgeni vibaya au kumdhulumu, kwa kuwa nanyi mlikuwa wageni huko Misri.
22“Usimdhulumu mjane wala yatima. 23Ukifanya hivyo nao wakinililia, hakika nitasikia kilio chao. 24Hasira yangu itawaka, nami nitawaua kwa upanga, wake zenu watakuwa wajane na watoto wenu watakuwa yatima.
25“Ukimkopesha mmoja wa watu wangu fedha ambaye ni mhitaji, usiwe kama mtu mkopesha fedha; usimtoze riba. 26Ukichukua vazi la jirani kama rehani, ulirudishe kwake kabla jua kuzama, 27kwa kuwa vazi lake ndilo pekee alilo nalo la kumfunika mwili wake. Ni nini kingine atajifunika nacho? Atakaponililia, nitasikia, kwa kuwa nina huruma.
28“Usimkufuru Mungu au kumlaani mtawala wa watu wako.
29“Usiache kutoa sadaka kutoka ghala lako au mapipa yako.
“Lazima unipe mzaliwa wa kwanza wa wana wako. 30Ufanye vivyo hivyo kwa ng’ombe wako na kwa kondoo wako. Waache wakae na mama zao kwa siku saba, lakini siku ya nane unipe.
31“Ninyi mtakuwa watu wangu watakatifu. Kwa hiyo msile nyama ya mnyama aliyeraruliwa na wanyama pori; mtupieni mbwa.

Iliyochaguliwa sasa

Kutoka 22: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia