Kutoka 23
23
Sheria za haki na rehema
1“Usieneze habari za uongo. Usimsaidie mtu mwovu kwa kuwa shahidi mwenye nia ya kudhuru wengine.
2“Usifuate umati wa watu katika kutenda mabaya. Unapotoa ushahidi kwenye mashtaka, usipotoshe haki ukijumuika na umati wa watu, 3nawe usimpendelee mtu maskini katika mashtaka yake.
4“Ukikutana na maksai au punda wa adui yako anapotea, hakikisha umemrudisha kwake. 5Ukiona punda wa mtu anayekuchukia ameanguka na mzigo wake, usimwache hapo alipoangukia; hakikisha kuwa umemsaidia.
6“Usiwanyime haki watu wako walio maskini katika mashtaka yao. 7Ujiepushe na mashtaka ya uongo, wala usimuue mtu asiye na hatia au mtu mwaminifu, kwa maana sitamhesabia hana hatia yeye aliye na hatia.
8“Usipokee rushwa, kwa kuwa rushwa hupofusha wale waonao, na kupinda maneno ya wenye haki.
9“Usimdhulumu mgeni; ninyi wenyewe mnajua jinsi mgeni anavyojisikia, kwa sababu mlikuwa wageni Misri.
Sheria za Sabato
10“Kwa muda wa miaka sita mtapanda mashamba yenu na kuvuna mazao, 11lakini katika mwaka wa saba usiilime ardhi wala kuitumia, ili watu walio maskini miongoni mwenu waweze kupata chakula kwenye hayo mashamba, nao wanyama pori wapate chakula kwa yale mabaki watakayobakiza. Utafanya hivyo katika shamba lako la mizabibu na la mizeituni.
12“Kwa siku sita fanya kazi zako, lakini siku ya saba usifanye kazi, ili maksai wako na punda wako wapate kupumzika, naye mtumwa aliyezaliwa nyumbani mwako, pamoja na mgeni, wapate kuburudishwa.
13“Uzingatie kutenda kila kitu nilichokuambia. Usiombe kwa majina ya miungu mingine, wala usiyaruhusu kusikika kinywani mwako.
Sikukuu tatu za mwaka
(Kutoka 34:18-26; Kumbukumbu 16:1-17)
14“Mara tatu kwa mwaka utanifanyia sikukuu.
15“Utaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu; kwa siku saba utakula mikate isiyotiwa chachu kama nilivyokuagiza. Fanya jambo hili kwa wakati uliopangwa katika mwezi wa Abibu#23:15 mwezi wa nne katika kalenda ya Kiyahudi, kwa sababu katika mwezi huo ulitoka Misri.
“Mtu yeyote asije mbele yangu mikono mitupu.
16“Utaadhimisha Sikukuu ya Mavuno kwa malimbuko ya mazao yako uliyopanda katika shamba lako.
“Utaadhimisha Sikukuu ya Kukusanya mavuno mwishoni mwa mwaka, unapokusanya mavuno yako toka shambani.
17“Mara tatu kwa mwaka wanaume wote watakuja mbele za Bwana Mungu Mwenyezi.
18“Msitoe damu ya dhabihu kwangu pamoja na kitu chochote kilicho na chachu.
“Mafuta ya mnyama wa sadaka ya sikukuu yangu yasibakizwe hadi asubuhi.
19“Utaleta malimbuko bora ya ardhi yako katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
“Usimchemshe mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.
Malaika wa Mwenyezi Mungu kuandaa njia
20“Tazama, ninamtuma malaika akutangulie mbele yako akulinde njiani na kukuleta mahali nilipoandaa. 21Mtamtii na kusikiliza kile anachokisema. Usiasi dhidi yake; hatakusamehe uasi wako, kwa maana Jina langu limo ndani yake. 22Ukizingatia atakachosema na kufanya yote ninayosema, nitakuwa adui wa adui zako, na nitawapinga wale wakupingao. 23Malaika wangu atatangulia mbele yako na kukuleta katika nchi ya Waamori, Wahiti, Waperizi, Wakanaani, Wahivi na Wayebusi, nami nitawafutilia mbali. 24Usiisujudie miungu yao, au kuiabudu, wala kufuata desturi yao. Utayabomoa kabisa na kuvunjavunja mawe yao ya ibada vipande vipande. 25Utamwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na baraka zake zitakuwa juu ya vyakula vyako na maji yako. Nami nitaondoa maradhi miongoni mwako, 26na hakuna atakayeharibu mimba wala atakayekuwa tasa katika nchi yako. Nami nitakupa maisha makamilifu.
27“Nitapeleka utisho wangu mbele yako na kufadhaisha kila taifa utakalolifikia. Nitafanya adui zako wote wakupe kisogo na kukimbia. 28Nitatanguliza nyigu mbele yako kuwafukuza Wahivi, Wakanaani na Wahiti waondoke njiani mwako. 29Lakini sitawafukuza kwa mara moja, kwa sababu nchi itabaki ukiwa na wanyama pori watakuwa wengi mno kwako. 30Nitawafukuza kidogo kidogo mbele yako, hadi uwe umeongezeka kiasi cha kutosha kuimiliki nchi.
31“Nitaweka mipaka ya nchi yako kuanzia Bahari ya Shamu hadi Bahari ya Wafilisti, na kuanzia jangwani hadi Mto#23:31 yaani Mto Frati. Nitawatia watu wanaoishi katika nchi hizo mikononi mwako, nawe utawafukuza watoke mbele yako. 32Usifanye agano lolote nao wala na miungu yao. 33Usiwaache waishi katika nchi yako, la sivyo watakusababisha utende dhambi dhidi yangu, kwa sababu ibada ya miungu yao hakika itakuwa mtego kwako.”
Iliyochaguliwa sasa
Kutoka 23: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.