Kutoka 21
21
Sheria mbalimbali
1“Hizi ndizo sheria utakazoweka mbele ya Waisraeli.
Watumishi wa Kiebrania
(Kumbukumbu 15:12-18)
2“Ukimnunua mtumwa Mwebrania, atakutumikia kwa miaka sita. Lakini katika mwaka wa saba, atakuwa huru naye ataenda zake pasipo kulipa chochote. 3Akija peke yake, ataenda huru peke yake, lakini akija na mke, ataondoka pamoja naye. 4Ikiwa bwana wake alimpatia mke naye akamzalia wana au binti, mwanamke pamoja na watoto wake watakuwa mali ya bwana wake, na huyo mwanaume ataondoka peke yake.
5“Lakini mtumishi akisema, ‘Ninampenda bwana wangu, mke wangu pamoja na watoto na sitaki kuwa huru,’ 6basi bwana wake atalazimika kumpeleka mbele ya waamuzi. Kisha atampeleka kwenye mlango, au kizingiti na kutoboa sikio lake kwa shazia. Naye atamtumikia bwana wake maisha yake yote.
7“Mtu akimuuza binti yake kuwa mtumwa, hataachwa huru kama watumwa wa kiume wanavyoachiwa. 8Kama hakumpendeza bwana wake aliyemchagua, huyo bwana atamwacha akombolewe. Hatakuwa na haki ya kumuuza kwa wageni, kwa sababu huyo bwana atakuwa amekosa uaminifu. 9Akimchagua aolewe na mwanawe, ni lazima ampe haki za kuwa binti yake. 10Ikiwa huyo mwana aliyeozwa mtumwa mwanamke ataoa mwanamke mwingine, ni lazima aendelee kumtosheleza huyo mke wa kwanza kwa chakula, mavazi na haki zote za ndoa. 11Iwapo hatamtosheleza kwa mambo hayo matatu, huyo mke wa kwanza ataondoka na kuwa huru bila malipo yoyote ya fedha.
Majeraha ya mwilini
12“Yeyote anayempiga mtu na kumuua ni lazima auawe. 13Hata hivyo, kama hakumuua kwa makusudi, lakini Mungu akaruhusu itendeke, basi atakimbilia mahali nitakapomchagulia. 14Lakini kama mtu akipanga na kumuua mwingine kwa makusudi, mwondoe katika madhabahu yangu na kumuua.
15“Yeyote anayemshambulia baba yake au mama yake ni lazima auawe.
16“Yeyote anayemteka nyara mwingine akamuuza au akamweka kwake, akikamatwa ni lazima auawe.
17“Yeyote atakayemlaani baba yake au mama yake ni lazima auawe.
18“Watu wakigombana, naye mmoja akampiga mwingine kwa jiwe au kwa ngumi yake na hakufa, bali akaugua na kulala kitandani, 19yule aliyempiga ngumi hatahesabiwa kuwa na hatia ikiwa mwenzake ataamka na kujikongoja kwa fimbo yake, lakini hata hivyo, ni lazima amlipe fidia ya muda aliopoteza na awajibike hadi apone kabisa.
20“Mtu akimpiga mtumwa wake wa kiume au wa kike kwa fimbo na mtumwa huyo akafa papo hapo, ni lazima aadhibiwe 21lakini ikiwa mtumwa ataamka baada ya siku moja au mbili, hataadhibiwa, kwa sababu yule mtumwa ni mali yake.
22“Watu wawili wakipigana na wakamuumiza mwanamke mjamzito, naye akazaa kabla ya wakati lakini hakuna majeraha makubwa, mhalifu atatozwa mali kiasi cha madai ya mume wa yule mwanamke, na jinsi mahakama itakavyoamua. 23Lakini kukiwa na jeraha kubwa, ni lazima ulipe uhai kwa uhai, 24jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu, 25kuchomwa moto kwa kuchomwa moto, jeraha kwa jeraha, mchubuko kwa mchubuko.
26“Mtu akimpiga mtumwa wa kiume au wa kike kwenye jicho na kuliharibu, ni lazima amwache huru yule mtumwa kama fidia ya hilo jicho. 27Akimvunja jino mtumwa wa kiume au wa kike, ni lazima amwache huru huyo mtumwa kwa kufidia hilo jino.
28“Fahali akimuua mwanaume au mwanamke kwa kumpiga kwa pembe, fahali huyo ni lazima auawe kwa kupigwa mawe, na nyama yake haitaliwa. Lakini mwenye fahali huyo hatawajibika. 29Lakini hata hivyo, ikiwa huyo fahali amekuwa na tabia ya kupiga kwa pembe, na mwenyewe ameonywa na hakutaka kumfungia naye akamuua mwanaume au mwanamke, huyo fahali ni lazima auawe kwa mawe na mwenye fahali pia auawe. 30Lakini ikiwa malipo yatatakiwa kwake, basi anaweza kulipa kinachodaiwa ili kuukomboa uhai wake. 31Sheria hii pia itatumika ikiwa fahali atampiga kwa pembe mwana au binti. 32Fahali akimpiga mtumwa wa kike au wa kiume, mwenye fahali atalipa shekeli thelathini#21:32 Shekeli 30 ni sawa na gramu 300. za fedha kwa bwana mwenye mtumwa, na fahali ni lazima auawe kwa mawe.
33“Mtu akiacha shimo wazi, ama akachimba shimo kisha asilifukie, na ng’ombe au punda akatumbukia ndani yake, 34mwenye shimo ni lazima alipe hasara iliyotokea; ni lazima amlipe mwenye mnyama. Mnyama aliyekufa atakuwa wake.
35“Fahali wa mtu fulani akimuumiza fahali wa mtu mwingine na akafa, watamuuza yule aliye hai na wagawane sawa fedha pamoja na mnyama aliyekufa. 36Hata hivyo, ikifahamika kwamba fahali huyo alikuwa na tabia ya kupiga kwa pembe na mwenyewe hakumfunga, ni lazima mwenye fahali alipe mnyama kwa mnyama, na mnyama aliyekufa atakuwa wake.
Iliyochaguliwa sasa
Kutoka 21: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.