Kutoka 20
20
Amri Kumi
(Kumbukumbu 5:1-21)
1Ndipo Mungu akasema maneno haya yote:
2“Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, niliyekutoa Misri, kutoka nchi ya utumwa.
3“Usiwe na miungu mingine ila mimi.
4Usijitengenezee sanamu katika umbo la kitu chochote kilicho juu mbinguni, au duniani chini, au ndani ya maji. 5Usivisujudie wala kuviabudu; kwa kuwa Mimi, Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi za baba zao hadi kizazi cha tatu na cha nne cha wanaonichukia, 6lakini ninaonesha upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanaonipenda na kuzishika amri zangu.
7Usilitaje bure jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa kuwa Mwenyezi Mungu hataacha kumhesabia hatia yeye alitajaye jina lake bure.
8Ikumbuke siku ya Sabato, uitakase. 9Kwa siku sita utafanya kazi na kutenda shughuli zako zote, 10lakini siku ya saba ni Sabato kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako. Siku hiyo hutafanya kazi yoyote, wewe, wala mwanao au binti yako, wala mtumishi wako wa kiume au wa kike, wala wanyama wako, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. 11Kwa kuwa kwa siku sita, Mwenyezi Mungu aliumba mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo, lakini akapumzika siku ya saba. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akaibariki siku ya Sabato na kuifanya takatifu.
12Waheshimu baba yako na mama yako, ili upate kuishi siku nyingi katika nchi anayokupa Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
13Usiue.
14Usizini.
15Usiibe.
16Usimshuhudie jirani yako uongo.
17Usiitamani nyumba ya jirani yako. Usimtamani mke wa jirani yako, wala mtumishi wake wa kiume au wa kike, wala ng’ombe wake au punda wake, wala chochote kile alicho nacho jirani yako.”
Watu wanaogopa
(Kumbukumbu 5:22-33)
18Watu walipoona ngurumo na radi, na kusikia mlio wa tarumbeta, na kuuona mlima katika moshi, walitetemeka kwa woga. Wakasimama mbali 19na wakamwambia Musa, “Sema nasi wewe mwenyewe, nasi tutakusikiliza. Lakini usimwache Mungu aseme nasi, la sivyo tutakufa.”
20Musa akawaambia watu, “Msiogope! Mungu amekuja kuwajaribu, ili hofu ya Mungu iwe nanyi kuwasaidia msitende dhambi.”
21Watu wakabaki mbali, wakati Musa alipolisogelea lile giza nene mahali pale Mungu alipokuwa.
Sanamu na madhabahu
22Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Waambie Waisraeli hivi: ‘Mmejionea wenyewe kwamba nimesema nanyi kutoka mbinguni: 23Msijifanyizie miungu yoyote na kuilinganisha nami, msijitengenezee miungu ya fedha wala miungu ya dhahabu.
24“ ‘Utanitengenezea madhabahu ya udongo, na juu yake utoe sadaka za kuteketezwa kwa moto na sadaka za amani, kondoo na mbuzi, na ng’ombe wako. Popote nitakapofanya Jina langu liheshimiwe, nitakuja kwenu na kuwabariki. 25Ikiwa unanitengenezea madhabahu ya mawe, usiijenge kwa mawe ya kuchonga, maana mkitumia chombo cha kuchongea mtaitia unajisi. 26Usitumie ngazi kupanda kwenye madhabahu yangu, uchi wako usije ukadhihirika kwa chini.’
Iliyochaguliwa sasa
Kutoka 20: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.