Kutoka 29:1-9
Kutoka 29:1-9 NENO
“Hili ndilo utakalofanya ili kuwaweka wakfu makuhani ili wanitumikie mimi katika kazi ya ukuhani: Chukua fahali mchanga mmoja na kondoo dume wawili wasio na dosari. Kutokana na unga laini wa ngano usiotiwa chachu, tengeneza mikate na maandazi yaliyokandwa kwa mafuta, pamoja na mikate myembamba iliyopakwa mafuta. Viwekwe vyote ndani ya kikapu na kuvitoa pamoja na yule fahali na wale kondoo dume wawili. Kisha mlete Haruni na wanawe kwenye lango la Hema la Kukutania na uwaoshe kwa maji. Chukua yale mavazi na umvike Haruni koti, joho la kizibau, na kizibau chenyewe, pamoja na kile kifuko cha kifuani. Mfungie hicho kizibau kwa ule mshipi wa kiunoni uliofumwa kwa ustadi. Weka kilemba kichwani mwake na kuweka taji takatifu lishikamane na hicho kilemba. Chukua yale mafuta ya upako umimine juu ya kichwa chake. Walete wanawe na uwavike makoti, pia uwavike zile tepe za kichwani. Ndipo uwafunge Haruni na wanawe mishipi. Ukuhani ni wao kwa agizo la kudumu. Kwa njia hii utamweka wakfu Haruni na wanawe.