Kutoka 29:1-9
Kutoka 29:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
“Haya ndiyo mambo utakayowafanyia Aroni na wanawe ili kuwaweka wakfu wanitumikie kama makuhani. Utachukua ndama dume na kondoo madume wawili wasio na dosari, mikate isiyotiwa chachu, maandazi yasiyotiwa chachu yaliyokandwa kwa mafuta, na mikate myembamba isiyotiwa chachu, lakini iliyopakwa mafuta. Vyote hivi viwe vimetengenezwa kwa unga laini wa ngano. Kisha iweke hiyo mikate ndani ya kikapu kimoja na kunitolea wakati mmoja na yule ndama dume na wale kondoo dume wawili. “Kisha wapeleke Aroni na wanawe mlangoni pa hema la mkutano na kuwatawadha. Kisha utachukua yale mavazi ya kikuhani umvike Aroni: Joho, kanzu, kizibao, kifuko cha kifuani, na kumfunga ule mshipi uliofumwa kwa ustadi. Tena utamvika kile kilemba kichwani na kuweka juu ya hicho kilemba ile taji takatifu. Baada ya kufanya hivyo, utachukua yale mafuta ya kupaka, ummiminie Aroni kichwani mwake kumweka wakfu. “Kisha utawaleta wana wa Aroni na kuwavika vizibao. Utawafunga mishipi viunoni na kuwavisha kofia zao. Hivyo ndivyo utakavyowaweka wakfu Aroni na wanawe kuwa makuhani. Hao watakuwa makuhani daima.
Kutoka 29:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nawe uwafanyie jambo hili, ili kuwaweka wakfu, wapate kunitumikia mimi katika kazi ya ukuhani; twaa njeku mmoja, na kondoo dume wawili wasio na dosari, na mkate usiotiwa chachu, na maandazi yasiyotiwa chachu yaliyokandwa kwa mafuta, na kaki zisizotiwa chachu zilizotiwa mafuta; utazifanya za unga mzuri mwembamba wa ngano. Nawe vitie vyote katika kikapu, uvilete ndani ya kikapu, pamoja na huyo ng'ombe, na hao kondoo dume wawili. Kisha mlete Haruni na wanawe hata mlangoni pa hema ya kukutania, ukawaoshe kwa maji. Kisha twaa hayo mavazi na kumvika Haruni; itie kanzu, na joho la naivera, na naivera, na kifuko cha kifuani, na kumkaza kwa huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi; nawe mvike kile kilemba kichwani, na lile taji takatifu utalitia katika kile kilemba. Ndipo utakapotwaa hayo mafuta ya kupaka, na kummiminia kichwani mwake, na kumtia mafuta. Kisha walete hao wanawe na kuwavika kanzu. Nawe uwakaze mishipi, Haruni na wanawe, na kuwavika kofia; nao watakuwa na huo ukuhani kwa amri ya milele; nawe utawaweka Haruni na wanawe kwa kazi takatifu.
Kutoka 29:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nawe uwafanyie jambo hili, ili kuwatakasa, wapate kunitumikia mimi katika kazi ya ukuhani; twaa ng’ombe mmoja mume kijana, na kondoo waume wawili walio wakamilifu, na mkate usiotiwa chachu, na maandazi yasiyotiwa chachu yaliyokandwa kwa mafuta, na kaki zisizotiwa chachu zilizotiwa mafuta; utazifanya za unga mzuri mwembamba wa ngano. Nawe vitie vyote katika kikapu, uvilete ndani ya kikapu, pamoja na huyo ng’ombe, na hao kondoo waume wawili. Kisha mlete Haruni na wanawe hata mlangoni pa hema ya kukutania, ukawaoshe kwa maji. Kisha twaa hayo mavazi na kumvika Haruni; itie kanzu, na joho ya naivera, na naivera, na kifuko cha kifuani, na kumkaza kwa huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi; nawe mvike kile kilemba kichwani, na ile taji takatifu utaitia katika kile kilemba. Ndipo utakapotwaa hayo mafuta ya kutiwa, na kummiminia kichwani mwake, na kumtia mafuta. Kisha walete hao wanawe na kuwavika kanzu. Nawe uwakaze mishipi, Haruni na wanawe, na kuwavika kofia; nao watakuwa na huo ukuhani kwa amri ya milele; nawe utawaweka Haruni na wanawe kwa kazi takatifu.
Kutoka 29:1-9 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Hili ndilo utakalofanya ili kuwaweka wakfu makuhani ili wanitumikie mimi katika kazi ya ukuhani: Chukua fahali mchanga mmoja na kondoo dume wawili wasio na dosari. Kutokana na unga laini wa ngano usiotiwa chachu, tengeneza mikate na maandazi yaliyokandwa kwa mafuta, pamoja na mikate myembamba iliyopakwa mafuta. Viwekwe vyote ndani ya kikapu na kuvitoa pamoja na yule fahali na wale kondoo dume wawili. Kisha mlete Haruni na wanawe kwenye lango la Hema la Kukutania na uwaoshe kwa maji. Chukua yale mavazi na umvike Haruni koti, joho la kizibau, na kizibau chenyewe, pamoja na kile kifuko cha kifuani. Mfungie hicho kizibau kwa ule mshipi wa kiunoni uliofumwa kwa ustadi. Weka kilemba kichwani mwake na kuweka taji takatifu lishikamane na hicho kilemba. Chukua yale mafuta ya upako umimine juu ya kichwa chake. Walete wanawe na uwavike makoti, pia uwavike zile tepe za kichwani. Ndipo uwafunge Haruni na wanawe mishipi. Ukuhani ni wao kwa agizo la kudumu. Kwa njia hii utamweka wakfu Haruni na wanawe.