Kutoka 32:7-18
Kutoka 32:7-18 NENO
Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Shuka, kwa sababu watu wako, uliowatoa Misri, wamepotoka. Wamekuwa wepesi kugeuka na kuacha niliyowaamuru, na wamejitengenezea sanamu ya kusubu yenye umbo la ndama. Wameisujudia na kuitolea dhabihu, nao wamesema, ‘Hii ndiyo miungu yenu, ee Israeli iliyokupandisha kutoka Misri.’ ” Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nimeona watu hawa, nao ni watu wenye shingo ngumu. Sasa niache ili hasira yangu ipate kuwaka dhidi yao, nami nipate kuwaangamiza. Kisha nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa.” Lakini Musa akamsihi Mwenyezi Mungu, Mungu wake, akasema, “Ee Mwenyezi Mungu, kwa nini hasira yako iwake dhidi ya watu wako, wale uliowatoa Misri kwa uweza mkuu na mkono wenye nguvu? Kwa nini Wamisri waseme, ‘Ni kwa nia mbaya aliwatoa Misri, ili awaue milimani na kuwafuta usoni mwa dunia’? Achilia mbali hasira yako kali, waonee huruma na usilete maafa juu ya watu wako. Wakumbuke watumishi wako Ibrahimu, Isaka na Israeli, ambao uliwaapia kwa nafsi yako mwenyewe: ‘Nitawafanya uzao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa wazao wako nchi hii yote niliyowaahidia, nayo itakuwa urithi wao milele.’ ” Kisha Mwenyezi Mungu akawaonea huruma, wala hakuleta juu ya watu wake maafa aliyokuwa amekusudia. Musa akageuka, akateremka kutoka mlimani akiwa na vile vibao viwili vya Ushuhuda mikononi mwake. Vilikuwa vimeandikwa pande zote mbili, mbele na nyuma. Vibao hivyo vilikuwa kazi ya Mungu; maandishi yalikuwa mwandiko wa Mungu, yaliyochorwa kama muhuri juu ya vibao. Yoshua aliposikia sauti za watu wakipiga kelele, akamwambia Musa, “Kuna sauti ya vita kambini.” Musa akajibu: “Si sauti ya ushindi, wala si sauti ya kushindwa; ni sauti ya kuimba ninayosikia.”