Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 32:7-18

Kutoka 32:7-18 SRUV

BWANA akamwambia Musa, Haya! Shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao, wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu wakasema, “Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri”. Tena BWANA akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, ni watu wakaidi basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize, nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu. Musa akamsihi sana BWANA, Mungu wake, na kusema, BWANA, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu? Kwa nini Wamisri waseme, kuwa “Amewatoa ili awatende mabaya, apate kuwaua milimani na kuwaangamiza watoke juu ya uso wa nchi?” Geuza katika hasira yako kali, ughairi uovu huu ulio nao juu ya watu wako. Mkumbuke Abrahamu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, Nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu nao watairithi milele. Na BWANA akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake. Basi, Musa akageuka akashuka katika mlima, na zile mbao mbili za mawe mikononi mwake; mbao zilizoandikwa pande zote mbili, upande huu na upande huu ziliandikwa. Na zile mbao zilikuwa kazi ya Mungu nayo maandiko yalikuwa maandiko ya Mungu, yaliyochorwa katika zile mbao. Na Yoshua aliposikia kelele za watu walipokuwa wakipiga kelele, akamwambia Musa, Kuna kelele ya vita kambini. Akasema, Hiyo si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushinda vitani, wala si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushindwa; bali kelele za watu waimbao ndizo ninazozisikia mimi.

Soma Kutoka 32