Kutoka 34:1-9
Kutoka 34:1-9 NENO
Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Chonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, nami nitaandika juu yake maneno yale yaliyokuwa kwenye vile vibao vya kwanza, ulivyovivunja. Uwe tayari asubuhi, kisha upande juu ya Mlima Sinai. Uje mbele zangu kukutana nami huko juu ya mlima. Mtu yeyote asije nawe, wala asionekane mtu popote mlimani; wala kondoo na mbuzi au ng’ombe wasilishe mbele ya huo mlima.” Kwa hiyo Musa akachonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, naye akapanda juu ya Mlima Sinai asubuhi na mapema, kama Mwenyezi Mungu alivyokuwa amemwagiza, akachukua vile vibao viwili vya mawe mikononi mwake. Kisha Mwenyezi Mungu akashuka katika wingu akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina lake, Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu akapita mbele ya Musa, akitangaza, “Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu, Mungu mwenye huruma na neema, asiye mwepesi wa hasira, mwingi wa upendo na uaminifu, akidumisha upendo kwa maelfu, pia akisamehe uovu, uasi na dhambi. Lakini haachi kuadhibu mwenye hatia; huwaadhibu watoto na watoto wao kwa ajili ya dhambi ya baba zao hata katika kizazi cha tatu na cha nne.” Mara Musa akasujudu na kuabudu. Musa akasema, “Ee Bwana, kama nimepata kibali mbele zako, basi Bwana uende pamoja nasi. Ingawa watu hawa ni wenye shingo ngumu, samehe uovu wetu na dhambi yetu, tuchukue kuwa urithi wako.”