Kutoka 34
34
Vibao vipya vya mawe
(Kumbukumbu 10:1-5)
1Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Chonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, nami nitaandika juu yake maneno yale yaliyokuwa kwenye vile vibao vya kwanza, ulivyovivunja. 2Uwe tayari asubuhi, kisha upande juu ya Mlima Sinai. Uje mbele zangu kukutana nami huko juu ya mlima. 3Mtu yeyote asije nawe, wala asionekane mtu popote mlimani; wala kondoo na mbuzi au ng’ombe wasilishe mbele ya huo mlima.”
4Kwa hiyo Musa akachonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, naye akapanda juu ya Mlima Sinai asubuhi na mapema, kama Mwenyezi Mungu alivyokuwa amemwagiza, akachukua vile vibao viwili vya mawe mikononi mwake. 5Kisha Mwenyezi Mungu akashuka katika wingu akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina lake, Mwenyezi Mungu. 6Mwenyezi Mungu akapita mbele ya Musa, akitangaza, “Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu, Mungu mwenye huruma na neema, asiye mwepesi wa hasira, mwingi wa upendo na uaminifu, 7akidumisha upendo kwa maelfu, pia akisamehe uovu, uasi na dhambi. Lakini haachi kuadhibu mwenye hatia; huwaadhibu watoto na watoto wao kwa ajili ya dhambi ya baba zao hata katika kizazi cha tatu na cha nne.”
8Mara Musa akasujudu na kuabudu. 9Musa akasema, “Ee Bwana, kama nimepata kibali mbele zako, basi Bwana uende pamoja nasi. Ingawa watu hawa ni wenye shingo ngumu, samehe uovu wetu na dhambi yetu, tuchukue kuwa urithi wako.”
Kufanya agano upya
(Kutoka 23:14-19; Kumbukumbu 7:1-5; 16:1-17)
10Kisha Mwenyezi Mungu akasema: “Tazama, ninafanya agano nanyi. Mbele ya watu wako wote nitafanya maajabu ambayo hayajafanyika katika taifa lolote katika ulimwengu wote. Watu wale mnaoishi miongoni mwao wataona jinsi ilivyo ya kushangaza kazi nitakayowafanyia Mimi, Mwenyezi Mungu wenu. 11Tii yale ninayokuamuru leo. Tazama nawafukuza mbele yako Waamori, Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. 12Uwe mwangalifu, usifanye agano na wale wanaokaa katika nchi ile unayoiendea, la sivyo watakuwa mtego katikati yako. 13Bomoa madhabahu yao, vunja mawe yao ya kuabudia, na ukatekate nguzo zao za Ashera. 14Usiabudu mungu mwingine, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, ambaye jina lake ni Wivu, ni Mungu mwenye wivu.
15“Uwe mwangalifu usifanye agano na wale watu wanaoishi katika nchi, kwa maana wakati wanapojifanyia ukahaba kwa miungu yao na kuwatolea kafara, watakualika wewe, nawe utakula sadaka za matambiko yao. 16Unapowachagua baadhi ya binti zao kuwa wake wa wana wenu na binti hao wakajifanyia ukahaba kwa miungu yao, watawaongoza wana wenu kufanya vivyo hivyo.
17“Usijifanyie sanamu za kusubu.
18“Utaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, kama nilivyokuamuru. Fanya hivi kwa wakati ulioamriwa, katika mwezi wa Abibu, ndio mwezi wa nne, kwa kuwa katika mwezi huo ndipo wewe ulipotoka Misri.
19“Mzaliwa wa kwanza wa kila tumbo ni mali yangu, pamoja na wazaliwa wa kwanza wote wa kiume wa mifugo yako, ikiwa ni wa ng’ombe au wa kondoo au mbuzi. 20Utakomboa mzaliwa wa kwanza wa punda kwa mwana-kondoo, lakini kama humkomboi, utavunja shingo yake. Utakomboa wazaliwa wako wa kwanza wote wa kiume.
“Mtu yeyote asije mbele zangu mikono mitupu.
21“Kwa siku sita utafanya kazi, lakini siku ya saba utapumzika, hata ikiwa ni majira ya kulima au ya kuvuna lazima upumzike.
22“Utaadhimisha Sikukuu ya Majuma kwa malimbuko ya mavuno ya ngano, na Sikukuu ya Mavuno mwishoni mwa mwaka. 23Mara tatu kwa mwaka wanaume wako wote watakuja mbele za Bwana Mungu Mwenyezi, Mungu wa Israeli. 24Nitawafukuza mataifa mbele yako na kupanua mipaka ya nchi yako, wala hakuna mtu yeyote atakayeitamani nchi yako wakati unapoenda mara tatu kila mwaka kuonana na Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
25“Usinitolee damu ya dhabihu pamoja na kitu chochote chenye chachu, wala usibakize dhabihu yoyote ya Sikukuu ya Pasaka hadi asubuhi.
26“Leta matunda ya kwanza yaliyo bora zaidi ya ardhi yako katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
“Usimchemshe mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.”
27Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Andika maneno haya, kwa maana kulingana na maneno haya, nimefanya agano na wewe pamoja na Israeli.” 28Musa alikuwa huko pamoja na Mwenyezi Mungu kwa siku arobaini usiku na mchana bila kula chakula wala kunywa maji. Naye akaandika juu ya vibao maneno ya agano, yaani zile Amri Kumi.
Mng’ao wa uso wa Musa
29Musa alipoteremka kutoka Mlima Sinai akiwa na vile vibao viwili vya Ushuhuda mikononi mwake, hakujua kuwa uso wake ulikuwa uking’aa, kwa sababu alikuwa amezungumza na Mwenyezi Mungu. 30Haruni na Waisraeli wote walipomwona Musa, kuwa uso wake unang’aa, waliogopa kumkaribia. 31Lakini Musa akawaita, kwa hiyo Haruni na viongozi wote wa jumuiya wakarudi, naye akazungumza nao. 32Baadaye Waisraeli wote wakamkaribia, naye akawapa amri zote Mwenyezi Mungu alizompa katika Mlima Sinai.
33Musa alipomaliza kuzungumza nao, akaweka utaji kwenye uso wake. 34Lakini kila wakati Musa alipoingia mbele za Mwenyezi Mungu kuzungumza naye, aliondoa ule utaji hadi alipotoka nje. Naye alipotoka nje na kuwaambia Waisraeli lile ambalo ameagizwa, 35waliona kuwa uso wake unang’aa. Kisha Musa angerudisha utaji juu ya uso wake hadi alipoingia ili kuzungumza na Mwenyezi Mungu.
Iliyochaguliwa sasa
Kutoka 34: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.