Kutoka 34:10-20
Kutoka 34:10-20 NEN
Kisha BWANA akasema: “Tazama ninafanya Agano mbele ya watu wako wote. Mbele ya watu wako wote nitafanya maajabu ambayo hayajafanyika katika taifa lolote katika ulimwengu wote. Watu wale mnaoishi miongoni mwao wataona jinsi ilivyo ya kushangaza ile kazi nitakayowafanyia mimi BWANA wenu. Tii yale ninayokuamuru leo. Tazama nawafukuza mbele yako Waamori, Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. Uwe mwangalifu, usifanye agano na wale wanaokaa katika nchi ile unayoiendea, la sivyo watakuwa mtego katikati yako. Bomoa madhabahu yao, vunja mawe yao ya kuabudia na ukatekate nguzo zao za Ashera. Usiabudu mungu mwingine, kwa kuwa BWANA, ambaye jina lake ni Wivu, ni Mungu mwenye wivu. “Uwe mwangalifu usifanye agano na wale watu wanaoishi katika nchi, kwa maana wakati wanapojifanyia ukahaba kwa miungu yao na kuwatolea kafara, watakualika wewe nawe utakula sadaka za matambiko yao. Unapowachagua baadhi ya binti zao kuwa wake wa wana wenu na binti hao wakajifanyia ukahaba kwa miungu yao, watawaongoza wana wenu kufanya vivyo hivyo. “Usijifanyie sanamu za kusubu. “Utaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, kama nilivyokuamuru. Fanya hivi kwa wakati ulioamriwa, katika mwezi wa Abibu, ndio mwezi wa nne, kwa kuwa katika mwezi huo ndipo wewe ulipotoka Misri. “Mzaliwa wa kwanza wa kila tumbo ni mali yangu, pamoja na wazaliwa wa kwanza wote wa kiume wa mifugo yako, ikiwa ni wa ngʼombe au wa kondoo au mbuzi. Utakomboa mzaliwa wa kwanza wa punda kwa mwana-kondoo, lakini kama humkomboi, utavunja shingo yake. Utakomboa wazaliwa wako wa kwanza wote wa kiume. “Mtu yeyote asije mbele zangu mikono mitupu.