Kutoka 38:21-31
Kutoka 38:21-31 NENO
Ifuatayo ni orodha ya vifaa vilivyotumika kwa ajili ya ujenzi wa maskani ya Mungu, hiyo Maskani ya Ushuhuda, ambavyo vilitayarishwa na Walawi kama alivyoagiza Musa, chini ya usimamizi wa Ithamari, mwana wa kuhani Haruni. (Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, alifanya kila kitu Mwenyezi Mungu alichomwamuru Musa, akiwa pamoja na Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, fundi stadi wa kutia nakshi, kubuni michoro, mtarizi kwa rangi ya buluu, ya zambarau, nyekundu na kitani safi.) Jumla ya dhahabu iliyopatikana kutokana na sadaka ya kuinuliwa kwa ajili ya kazi ya mahali patakatifu ilikuwa na uzito wa talanta ishirini na tisa na shekeli mia saba na thelathini (730), kulingana na shekeli ya mahali patakatifu. Fedha iliyopatikana kutokana na jumuiya ya watu waliohesabiwa ilikuwa yenye uzito wa talanta mia moja na shekeli elfu moja mia saba sabini na tano (1,775), kulingana na shekeli ya mahali patakatifu. Kila mtu alitoa beka moja, ambayo ni sawa na nusu shekeli ya fedha, kwa kazi ya mahali patakatifu, kutoka kwa kila mtu aliyekuwa amehesabiwa mwenye umri wa miaka ishirini au zaidi, ambao jumla yao walikuwa wanaume elfu mia sita na tatu mia tano na hamsini (603,550). Talanta hizo mia moja za fedha zilitumika kusubu vile vitako mia moja kwa ajili ya mahali patakatifu na pazia: vitako mia moja kwa talanta mia, yaani talanta moja kwa kila kitako. Akatumia hizo shekeli elfu moja mia saba sabini na tano (1,775) kutengeneza kulabu za nguzo, kufunika ncha za nguzo, na kutengeneza vitanzi vyake. Shaba iliyopatikana kutokana na sadaka ya kuinuliwa ilikuwa na uzito wa talanta sabini na shekeli elfu mbili mia nne. Akaitumia hiyo shaba kutengeneza vitako vya ingilio la Hema la Kukutania, madhabahu ya shaba pamoja na ule wavu wake na vyombo vyake vyote, vile vitako vya ule ua uliozunguka na vile vya ingilio, na vigingi vyote vya maskani ya Mungu, pamoja na vigingi vya ule ua uliozunguka.