Kutoka 4:10-17
Kutoka 4:10-17 NEN
Mose akamwambia BWANA, “Ee Bwana, kamwe sijapata kuwa msemaji kwa ufasaha wakati uliopita wala tangu ulipoanza kuzungumza na mtumishi wako. Ulimi wangu ni mzito kuzungumza.” BWANA akamwambia, “Ni nani aliyempa mwanadamu kinywa? Ni nani aliyemfanya mtu kuwa kiziwi au bubu? Ni nani anayempa mtu kuona au upofu? Je, si mimi, BWANA? Sasa nenda, nitakusaidia kusema, nami nitakufundisha jambo la kusema.” Lakini Mose akasema, “Ee Bwana, tafadhali mtume mtu mwingine kufanya kazi hiyo.” Ndipo hasira ya BWANA ikawaka dhidi ya Mose, akamwambia, “Vipi kuhusu ndugu yako, Aroni Mlawi? Ninajua yeye anaweza kuzungumza vizuri. Naye yuko tayari njiani kukulaki, na moyo wake utafurahi wakati atakapokuona. Utazungumza naye na kuweka maneno kinywani mwake. Nitawasaidia ninyi wawili kusema, nami nitawafundisha jambo la kufanya. Aroni ataongea na watu badala yako na itakuwa kwamba yeye amekuwa kinywa chako nawe utakuwa kama Mungu kwake. Lakini chukua fimbo hii mkononi mwako ili uweze kuitumia kufanya ishara hizo za ajabu.”