5
Matofali bila nyasi
1Baadaye Musa na Haruni wakaenda kwa Farao, wakamwambia, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Waruhusu watu wangu waende, ili waweze kunifanyia sikukuu huko jangwani.’ ”
2Farao akasema, “Huyo Mwenyezi Mungu ni nani, hata nimtii na kuruhusu Waisraeli waende? Simjui huyo Mwenyezi Mungu wala sitawaruhusu Waisraeli waende.”
3Ndipo Musa na Haruni wakasema, “Mungu wa Waebrania amekutana nasi. Sasa turuhusu tuwe na safari ya siku tatu ya jangwani ili tukamtolee Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, dhabihu, la sivyo aweza kutupiga sisi kwa tauni au kwa upanga.”
4Lakini mfalme wa Misri akasema, “Mbona ninyi Musa na Haruni mnawaondoa watu kutoka kwenye kazi zao? Rudini kwenye kazi zenu!” 5Kisha Farao akasema, “Tazama, sasa watu hawa ni wengi, nanyi mnawazuia kufanya kazi.”
6Siku hiyo hiyo, Farao akatoa amri hii kwa viongozi wa watumwa na wasimamizi wa watu, akawaambia: 7“Tangu sasa msiwape hawa watu nyasi za kutengenezea matofali; wakusanye nyasi zao wenyewe. 8Lakini watakeni kutengeneza matofali kiasi kile kile cha mwanzo, kiwango kisipunguzwe. Wao ni wavivu, ndiyo sababu wanalia, wakisema, ‘Turuhusiwe twende kumtolea Mungu wetu dhabihu.’ 9Fanyeni kazi kuwa ngumu zaidi kwa watu hao ili wakazane na kazi na kuacha kusikiliza uongo.”
10Basi viongozi wa watumwa na wasimamizi wakaenda kuwaambia watu, “Hivi ndivyo Farao asemavyo: ‘Sitawapa nyasi tena. 11Nendeni mkatafute nyasi wenyewe popote mnapoweza kuzipata, lakini kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo.’ ” 12Basi watu wakatawanyika kote nchini Misri kukusanya mabua ya kutumia badala ya nyasi. 13Viongozi wa watumwa wakasisitiza wakisema, “Timizeni kazi mnayotakiwa kwa kila siku, kama wakati ule mlipokuwa mkipewa nyasi.” 14Wasimamizi wa Waisraeli waliochaguliwa na viongozi wa watumwa wa Farao walipigwa na kuulizwa, “Kwa nini hamkutimiza kiwango chenu cha kutengeneza matofali jana na leo, kama mwanzoni?”
15Ndipo wasimamizi wa Waisraeli wakaenda kumlilia Farao, wakisema: “Mbona umewatendea watumishi wako hivi? 16Watumishi wako hawapewi nyasi, hata hivyo tumeambiwa, ‘Tengenezeni matofali!’ Watumishi wako wanapigwa, lakini kosa ni la watu wako wenyewe.”
17Farao akasema, “Ninyi ni wavivu ndiyo sababu mnasema, ‘Turuhusu twende tukamtolee Mwenyezi Mungu dhabihu.’ 18Sasa nendeni kazini. Hamtapewa nyasi zozote, nanyi ni lazima mtengeneze matofali.”
19Wasimamizi wa Waisraeli walitambua kuwa wako taabani walipoambiwa, “Hamtakiwi kupunguza idadi ya matofali mliotakiwa kutengeneza kila siku.” 20Walipoondoka kwa Farao, wakawakuta Musa na Haruni wakingojea kukutana nao, 21wakawaambia Musa na Haruni, “Mwenyezi Mungu na awaangalie awahukumu ninyi! Mmetufanya tuwe chukizo kwa Farao na maafisa wake, nanyi mmeweka upanga mikononi mwao ili kutuua sisi.”
Mwenyezi Mungu anaahidi ukombozi
22Musa akarudi kwa Mwenyezi Mungu na kumwambia, “Ee Bwana, mbona umewaletea watu hawa taabu? Kwa nini basi ukanituma mimi? 23Tangu nilipokwenda kuzungumza na Farao kwa jina lako, amewaletea watu hawa taabu, nawe kamwe hujawakomboa watu wako.”