Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 6

6
1Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Sasa utaona kitu nitakachomfanyia Farao: Kwa sababu ya mkono wangu wenye nguvu atawaachia watu waende; kwa sababu ya mkono wangu wenye nguvu atawafukuza waondoke nchini mwake.”
2Pia Mungu akamwambia Musa, “Mimi ndimi Mwenyezi Mungu. 3Nilimtokea Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo kama Mungu Mwenyezi#6:3 Kiebrania El-Shaddai (yaani Mungu Mwenye utoshelevu wote)., ingawa kwa Jina langu, Yehova, sikujitambulisha kwao. 4Pia niliweka agano langu nao kuwapa nchi ya Kanaani, ambako waliishi kama wageni. 5Zaidi ya hayo, nimesikia kilio cha huzuni cha Waisraeli ambao Wamisri wamewatia utumwani, nami nimelikumbuka agano langu.
6“Kwa hiyo, waambie Waisraeli: ‘Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nami nitawatoa katika nira ya Wamisri. Nitawaweka huru mtoke kuwa watumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyooshwa pamoja na matendo makuu ya hukumu. 7Nitawachukua ninyi kuwa watu wangu mwenyewe, nami nitakuwa Mungu wenu. Ndipo mtajua kuwa mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, niliyewatoa chini ya nira ya Wamisri. 8Nami nitawaleta hadi nchi niliyoapa kwa mkono ulioinuliwa kumpa Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Nitawapa iwe milki yenu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
9Musa akawaarifu Waisraeli jambo hili, lakini hawakumsikiliza kwa sababu ya kuvunjika moyo na kazi yao ngumu.
10Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 11“Nenda, mwambie Farao mfalme wa Misri awaachie Waisraeli waondoke nchini mwake.”
12Lakini Musa akamwambia Mwenyezi Mungu, “Ikiwa Waisraeli hawatanisikiliza, kwa nini yeye Farao anisikilize mimi, ambaye huzungumza kwa kigugumizi?”
Orodha ya jamaa ya Musa na Haruni
13Ndipo Mwenyezi Mungu akanena na Musa na Haruni kuhusu Waisraeli na Farao mfalme wa Misri, naye akawaamuru wawatoe Waisraeli kutoka Misri.
14Hawa walikuwa wakuu wa jamaa zao:
Wana wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa kiume wa Israeli walikuwa:
Hanoki na Palu, Hesroni na Karmi.
Hizo zilikuwa koo za Reubeni.
15Wana wa Simeoni walikuwa:
Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari na Shauli mwana wa mwanamke Mkanaani.
Hizo zilikuwa koo za Simeoni.
16Haya ndiyo majina ya wana wa Lawi, kulingana na orodha zao:
Gershoni, Kohathi na Merari.
Lawi aliishi miaka mia moja na thelathini na saba (137).
17Wana wa Gershoni kwa koo walikuwa:
Libni na Shimei.
18Wana wa Kohathi walikuwa:
Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli.
Kohathi aliishi miaka mia moja na thelathini na tatu (133).
19Wana wa Merari walikuwa:
Mahli na Mushi.
Hizo zilikuwa koo za Lawi, kulingana na orodha zao.
20Amramu akamwoa Yokebedi, shangazi yake, aliyemzalia Haruni na Musa.
Amramu aliishi miaka mia moja na thelathini na saba (137).
21Wana wa Ishari walikuwa:
Kora, Nefegi na Zikri.
22Wana wa Uzieli walikuwa:
Mishaeli, Elisafani na Sithri.
23Haruni akamwoa Elisheba binti Aminadabu, ndugu yake Nashoni, naye akamzalia Nadabu na Abihu, Eleazari na Ithamari.
24Wana wa Kora walikuwa:
Asiri, Elkana na Abiasafu.
Hizo zilikuwa koo za Kora.
25Eleazari mwana wa Haruni akamwoa mmoja wa binti za Putieli, naye akamzalia Finehasi.
Hao walikuwa wakuu wa jamaa za Walawi, kufuatana na koo zao.
26Hawa walikuwa Haruni na Musa, wale wale ambao Mwenyezi Mungu aliwaambia, “Watoeni Waisraeli katika nchi ya Misri kwa vikosi vyao.” 27Hao ndio waliozungumza na Farao, mfalme wa Misri kuhusu kuwatoa Waisraeli Misri. Ilikuwa ni huyo Musa na huyo Haruni.
Haruni kuzungumza badala ya Musa
28Mwenyezi Mungu aliponena na Musa huko Misri, 29akamwambia, “Mimi ndimi Mwenyezi Mungu. Mwambie Farao mfalme wa Misri kila kitu nikuambiacho.”
30Lakini Musa akamwambia Mwenyezi Mungu, “Kwa kuwa mimi huzungumza kwa kigugumizi, Farao atanisikiliza mimi?”

Iliyochaguliwa sasa

Kutoka 6: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia