Kutoka 6:9-25
Kutoka 6:9-25 NENO
Musa akawaarifu Waisraeli jambo hili, lakini hawakumsikiliza kwa sababu ya kuvunjika moyo na kazi yao ngumu. Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nenda, mwambie Farao mfalme wa Misri awaachie Waisraeli waondoke nchini mwake.” Lakini Musa akamwambia Mwenyezi Mungu, “Ikiwa Waisraeli hawatanisikiliza, kwa nini yeye Farao anisikilize mimi, ambaye huzungumza kwa kigugumizi?” Ndipo Mwenyezi Mungu akanena na Musa na Haruni kuhusu Waisraeli na Farao mfalme wa Misri, naye akawaamuru wawatoe Waisraeli kutoka Misri. Hawa walikuwa wakuu wa jamaa zao: Wana wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa kiume wa Israeli walikuwa: Hanoki na Palu, Hesroni na Karmi. Hizo zilikuwa koo za Reubeni. Wana wa Simeoni walikuwa: Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari na Shauli mwana wa mwanamke Mkanaani. Hizo zilikuwa koo za Simeoni. Haya ndiyo majina ya wana wa Lawi, kulingana na orodha zao: Gershoni, Kohathi na Merari. Lawi aliishi miaka mia moja na thelathini na saba (137). Wana wa Gershoni kwa koo walikuwa: Libni na Shimei. Wana wa Kohathi walikuwa: Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli. Kohathi aliishi miaka mia moja na thelathini na tatu (133). Wana wa Merari walikuwa: Mahli na Mushi. Hizo zilikuwa koo za Lawi, kulingana na orodha zao. Amramu akamwoa Yokebedi, shangazi yake, aliyemzalia Haruni na Musa. Amramu aliishi miaka mia moja na thelathini na saba (137). Wana wa Ishari walikuwa: Kora, Nefegi na Zikri. Wana wa Uzieli walikuwa: Mishaeli, Elisafani na Sithri. Haruni akamwoa Elisheba binti Aminadabu, ndugu yake Nashoni, naye akamzalia Nadabu na Abihu, Eleazari na Ithamari. Wana wa Kora walikuwa: Asiri, Elkana na Abiasafu. Hizo zilikuwa koo za Kora. Eleazari mwana wa Haruni akamwoa mmoja wa binti za Putieli, naye akamzalia Finehasi.