Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 7:14-25

Kutoka 7:14-25 NEN

Kisha BWANA akamwambia Mose, “Moyo wa Farao ni mgumu, anakataa kuwaachia watu kuondoka. Nenda kwa Farao asubuhi wakati anapokwenda mtoni. Ngoja ukingoni mwa Naili ili uonane naye, na uchukue mkononi mwako fimbo ile iliyobadilishwa kuwa nyoka. Kisha umwambie, ‘BWANA, Mungu wa Waebrania, amenituma nikuambie: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu jangwani. Lakini hadi sasa hujasikiliza. Hili ndilo BWANA asemalo: Kwa hili utajua kuwa Mimi ndimi BWANA: Fimbo iliyo mkononi mwangu nitapiga nayo maji ya Naili nayo yatabadilika kuwa damu. Samaki waliomo katika Mto Naili watakufa, nao mto utanuka vibaya, Wamisri hawataweza kunywa hayo maji yake.’ ” BWANA akamwambia Mose, “Mwambie Aroni, ‘Chukua ile fimbo yako unyooshe mkono wako juu ya maji ya Misri, juu ya chemchemi na mifereji, juu ya madimbwi na mabwawa yote,’ navyo vitabadilika kuwa damu. Damu itakuwa kila mahali katika Misri, hata kwenye vyombo vya miti na vya mawe.” Mose na Aroni wakafanya kama vile BWANA alivyokuwa amewaagiza. Akainua fimbo yake machoni pa Farao na maafisa wake na kuyapiga maji ya Mto Naili, na maji yote yakabadilika kuwa damu. Samaki katika Mto Naili wakafa, nao mto ukanuka vibaya sana kiasi kwamba Wamisri hawakuweza kunywa maji yake. Damu ilikuwa kila mahali katika nchi ya Misri. Lakini waganga wa Misri kwa kutumia siri ya uganga wao wakafanya vivyo hivyo, nao moyo wa Farao ukawa mgumu, hakuwasikiliza Mose na Aroni, kama vile BWANA alivyokuwa amesema. Badala yake, Farao akageuka, akaenda kwenye jumba lake la kifalme, wala hakulitia hili moyoni. Nao Wamisri wote wakachimba kandokando ya Mto Naili kupata maji ya kunywa, kwa sababu hawakuweza kunywa maji ya mto. Zilipita siku saba baada ya BWANA kuyapiga maji ya Mto Naili.