Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 7:14-25

Kutoka 7:14-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

BWANA akamwambia Musa, Moyo wa Farao ni mzito, anakataa kuwapa watu ruhusa waende zao. Mwendee Farao asubuhi; tazama, atoka kwenda majini; nawe simama karibu na ufuo wa mto ili upate kuonana naye; na ile fimbo iliyogeuzwa kuwa nyoka utaichukua mkononi mwako. Nawe umwambie, BWANA, Mungu wa Waebrania, amenituma nije kwako, kusema, Wape watu wangu ruhusa, ili wapate kunitumikia jangwani; nawe, tazama! Hujasikia hata sasa. BWANA asema, Katika jambo hili utanijua ya kuwa mimi ndimi BWANA; tazama, nitayapiga haya maji yaliyo mtoni kwa fimbo hii niliyo nayo mkononi mwangu, nayo yatageuzwa kuwa damu. Na hao samaki walio mtoni watakufa, na huo mto utatoa uvundo; nao Wamisri watachukizwa kuyanywa maji ya mtoni. BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Shika fimbo yako, kaunyoshe mkono wako juu ya maji ya Misri, juu ya mito yao, juu ya vijito vyao, na juu ya maziwa ya maji yao, na juu ya visima vyao vyote vya maji, ili yageuke kuwa damu, nako kutakuwa na damu katika nchi yote ya Misri, katika vyombo vya mti, na katika vyombo vya jiwe. Musa na Haruni wakafanya hivyo, kama BWANA alivyowaambia; naye akaiinua ile fimbo, na kuyapiga maji yaliyokuwa mtoni, mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake; na hayo maji yote yaliyokuwa katika mto yakageuzwa kuwa damu. Hao samaki waliokuwa mtoni nao wakafa; na ule mto ukatoa uvundo, Wamisri wasipate kunywa maji ya mtoni; na ile damu ilikuwa katika nchi yote na Misri. Lakini waganga wa Misri wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao; na moyo wake Farao ukawa mgumu, wala hakuwasikiza, kama BWANA alivyonena. Farao akazunguka na kuingia nyumbani mwake, wala hata hilo hakuliweka moyoni. Wamisri wote wakachimba-chimba kando ya mto ili wapate maji ya kunywa; maana, hawakuweza kuyanywa yale maji ya mtoni. Zikatimia siku saba, baada ya BWANA kuupiga ule mto.

Shirikisha
Soma Kutoka 7

Kutoka 7:14-25 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Moyo wa Farao umekuwa mgumu. Anakataa kuwaacha Waisraeli waondoke. Basi, nenda ukakutane naye kesho asubuhi, wakati anapokwenda mtoni Nili. Mngojee kando ya mto. Chukua mkononi mwako ile fimbo iliyogeuka kuwa nyoka. Kisha mwambie hivi, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, amenituma kwako, naye asema hivi, ‘Waache watu wangu waende zao ili wanitumikie jangwani, lakini mpaka sasa wewe hupendi kutii. Basi, Mwenyezi-Mungu asema kwamba sasa utamtambua yeye ni nani. Nitayapiga maji ya mto Nili kwa fimbo hii, na maji yote yatageuka kuwa damu. Samaki waliomo mtoni Nili watakufa, mto wote utanuka vibaya, na Wamisri watachukia kabisa kunywa maji yake.’” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mwambie Aroni aichukue fimbo yake na kuinyosha juu ya maji ya Misri, juu ya mito yote, mifereji, madimbwi na mabwawa yao yote, nayo yatakuwa damu. Kutakuwa na damu nchini kote, na hata katika vyombo vyote vya mbao na vya mawe.” Mose na Aroni wakafanya kama Mwenyezi-Mungu alivyowaamuru. Aroni aliinua fimbo yake juu mbele ya Farao na maofisa wake, akayapiga maji ya mto Nili, na maji yote mtoni yakageuka kuwa damu. Samaki wakafa, mto ukanuka vibaya sana hata Wamisri wasiweze kunywa maji yake. Nchi nzima ikajaa damu. Lakini wachawi wa Misri kwa kutumia uchawi wao wakafanya vivyo hivyo. Kwa hiyo moyo wa Farao ukabaki kuwa mgumu, naye hakuwasikiliza Mose na Aroni; ikawa kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa amesema. Basi, Farao akarudi nyumbani kwake, na hata haya yaliyotokea hakuyajali. Wamisri wote wakachimbachimba kandokando ya mto Nili ili wapate maji ya kunywa, kwani hawakuweza kunywa maji ya mto huo. Pigo hilo la mto Nili lilidumu siku saba.

Shirikisha
Soma Kutoka 7

Kutoka 7:14-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)

BWANA akamwambia Musa, Moyo wa Farao ni mzito, anakataa kuwapa watu ruhusa waende zao. Mwendee Farao asubuhi; tazama, atoka kwenda majini; nawe simama karibu na ufuo wa mto ili upate kuonana naye; na ile fimbo iliyogeuzwa kuwa nyoka utaichukua mkononi mwako. Nawe umwambie, BWANA, Mungu wa Waebrania, amenituma nije kwako, kusema, Wape watu wangu ruhusa, ili wapate kunitumikia jangwani; nawe, tazama! Hujasikia hata sasa. BWANA asema, Katika jambo hili utanijua ya kuwa mimi ndimi BWANA; tazama, nitayapiga haya maji yaliyo mtoni kwa fimbo hii niliyo nayo mkononi mwangu, nayo yatageuzwa kuwa damu. Na hao samaki walio mtoni watakufa, na huo mto utatoa uvundo; nao Wamisri watachukizwa kuyanywa maji ya mtoni. BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Shika fimbo yako, kaunyoshe mkono wako juu ya maji ya Misri, juu ya mito yao, juu ya vijito vyao, na juu ya maziwa ya maji yao, na juu ya visima vyao vyote vya maji, ili yageuke kuwa damu, nako kutakuwa na damu katika nchi yote ya Misri, katika vyombo vya mti, na katika vyombo vya jiwe. Musa na Haruni wakafanya hivyo, kama BWANA alivyowaambia; naye akaiinua ile fimbo, na kuyapiga maji yaliyokuwa mtoni, mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake; na hayo maji yote yaliyokuwa katika mto yakageuzwa kuwa damu. Hao samaki waliokuwa mtoni nao wakafa; na ule mto ukatoa uvundo, Wamisri wasipate kunywa maji ya mtoni; na ile damu ilikuwa katika nchi yote ya Misri. Lakini waganga wa Misri wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao; na moyo wake Farao ukawa mgumu, wala hakuwasikiza, kama BWANA alivyonena. Farao akazunguka na kuingia nyumbani mwake, wala hata hilo hakuliweka moyoni. Wamisri wote wakachimbachimba kando ya mto ili wapate maji ya kunywa; maana, hawakuweza kuyanywa yale maji ya mtoni. Zikatimia siku saba, baada ya BWANA kuupiga ule mto.

Shirikisha
Soma Kutoka 7

Kutoka 7:14-25 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kisha BWANA akamwambia Mose, “Moyo wa Farao ni mgumu, anakataa kuwaachia watu kuondoka. Nenda kwa Farao asubuhi wakati anapokwenda mtoni. Ngoja ukingoni mwa Naili ili uonane naye, na uchukue mkononi mwako fimbo ile iliyobadilishwa kuwa nyoka. Kisha umwambie, ‘BWANA, Mungu wa Waebrania, amenituma nikuambie: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu jangwani. Lakini hadi sasa hujasikiliza. Hili ndilo BWANA asemalo: Kwa hili utajua kuwa Mimi ndimi BWANA: Fimbo iliyo mkononi mwangu nitapiga nayo maji ya Naili nayo yatabadilika kuwa damu. Samaki waliomo katika Mto Naili watakufa, nao mto utanuka vibaya, Wamisri hawataweza kunywa hayo maji yake.’ ” BWANA akamwambia Mose, “Mwambie Aroni, ‘Chukua ile fimbo yako unyooshe mkono wako juu ya maji ya Misri, juu ya chemchemi na mifereji, juu ya madimbwi na mabwawa yote,’ navyo vitabadilika kuwa damu. Damu itakuwa kila mahali katika Misri, hata kwenye vyombo vya miti na vya mawe.” Mose na Aroni wakafanya kama vile BWANA alivyokuwa amewaagiza. Akainua fimbo yake machoni pa Farao na maafisa wake na kuyapiga maji ya Mto Naili, na maji yote yakabadilika kuwa damu. Samaki katika Mto Naili wakafa, nao mto ukanuka vibaya sana kiasi kwamba Wamisri hawakuweza kunywa maji yake. Damu ilikuwa kila mahali katika nchi ya Misri. Lakini waganga wa Misri kwa kutumia siri ya uganga wao wakafanya vivyo hivyo, nao moyo wa Farao ukawa mgumu, hakuwasikiliza Mose na Aroni, kama vile BWANA alivyokuwa amesema. Badala yake, Farao akageuka, akaenda kwenye jumba lake la kifalme, wala hakulitia hili moyoni. Nao Wamisri wote wakachimba kandokando ya Mto Naili kupata maji ya kunywa, kwa sababu hawakuweza kunywa maji ya mto. Zilipita siku saba baada ya BWANA kuyapiga maji ya Mto Naili.

Shirikisha
Soma Kutoka 7