Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 7

7
1Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Tazama, nimekufanya kama Mungu kwa Farao, naye Haruni ndugu yako atakuwa nabii wako. 2Utasema kila kitu nitakachokuagiza, naye Haruni ndugu yako atamwambia Farao awaachie Waisraeli watoke katika nchi yake. 3Lakini nitaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu. Ingawa nitazidisha ishara na maajabu katika Misri, 4hatawasikiliza. Kisha nitaupeleka mkono wangu juu ya Misri, na kwa matendo makuu ya hukumu nitavitoa vikosi vyangu, watu wangu Waisraeli. 5Nao Wamisri watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu nitakapounyoosha mkono wangu dhidi ya Misri na kuwatoa Waisraeli humo.”
6Musa na Haruni wakafanya sawasawa na jinsi Mwenyezi Mungu alivyowaamuru. 7Musa alikuwa na umri wa miaka themanini na Haruni alikuwa na umri wa miaka themanini na tatu walipozungumza na Farao.
Fimbo ya Haruni yawa nyoka
8Mwenyezi Mungu akamwambia Musa na Haruni, 9“Farao atakapowaambia, ‘Fanyeni muujiza,’ basi mwambie Haruni, ‘Chukua fimbo yako na uitupe chini mbele ya Farao,’ nayo fimbo itakuwa nyoka.”
10Ndipo Musa na Haruni wakaenda kwa Farao, wakafanya sawasawa na jinsi Mwenyezi Mungu alivyoagiza. Haruni akaitupa ile fimbo yake chini mbele ya Farao na maafisa wake, nayo ikawa nyoka. 11Farao naye akawaita watu wenye maarifa na wachawi na waganga wa Misri, nao wakafanya vivyo hivyo kwa siri ya uganga wao. 12Kila mmoja alitupa fimbo yake chini, nayo ikawa nyoka. Lakini fimbo ya Haruni ikazimeza zile fimbo zao. 13Hata hivyo, moyo wa Farao ukawa mgumu, naye hakuwasikiliza Musa na Haruni, kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema.
Pigo la kwanza: Damu
14Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Moyo wa Farao ni mgumu; anakataa kuwaacha watu waondoke. 15Nenda kwa Farao asubuhi anapoenda mtoni. Ngoja ukingoni mwa Mto Naili ili uonane naye, na uchukue mkononi mwako fimbo ile iliyobadilishwa kuwa nyoka. 16Kisha umwambie, ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wa Waebrania, amenituma nikuambie: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu jangwani. Lakini hadi sasa hujasikiliza. 17Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Kwa hili utajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu: Kwa fimbo iliyo mkononi mwangu nitapiga maji ya Mto Naili, nayo yatabadilika kuwa damu. 18Samaki walio katika Mto Naili watakufa, nao mto utanuka vibaya; Wamisri hawataweza kunywa maji yake.’ ”
19Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Mwambie Haruni, ‘Chukua ile fimbo yako unyooshe mkono wako juu ya maji ya Misri, juu ya chemchemi na mifereji, juu ya madimbwi na mabwawa yote,’ navyo vitabadilika kuwa damu. Damu itakuwa kila mahali katika Misri, hata kwenye vyombo vya miti na vya mawe.”
20Musa na Haruni wakafanya kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amewaagiza. Akainua fimbo yake machoni pa Farao na maafisa wake na kuyapiga maji ya Mto Naili, na maji yote yakabadilika kuwa damu. 21Samaki katika Mto Naili wakafa, nao mto ukanuka vibaya sana kiasi kwamba Wamisri hawakuweza kunywa maji yake. Damu ilikuwa kila mahali katika nchi ya Misri.
22Lakini waganga wa Misri kwa kutumia siri ya uganga wao wakafanya vivyo hivyo, nao moyo wa Farao ukawa mgumu, hakuwasikiliza Musa na Haruni, kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema. 23Badala yake, Farao akageuka, akaenda kwenye jumba lake la kifalme, wala hakulitia hili moyoni. 24Nao Wamisri wote wakachimba kandokando ya Mto Naili kupata maji ya kunywa, kwa sababu hawakuweza kunywa maji ya mto.
Pigo la pili: Vyura
25Zilipita siku saba baada ya Mwenyezi Mungu kuyapiga maji ya Mto Naili.

Iliyochaguliwa sasa

Kutoka 7: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia