Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 12:1-16

Ezekieli 12:1-16 NENO

Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: “Mwanadamu, unaishi miongoni mwa watu waasi. Wana macho ya kuona, lakini hawaoni, na masikio ya kusikia lakini hawasikii, kwa kuwa ni watu waasi. “Kwa hiyo, mwanadamu, funga mizigo yako kwa kwenda uhamishoni tena wakati wa mchana, wakiwa wanakutazama, toka nje na uende mahali pengine kutoka hapo ulipo. Huenda wataelewa, ingawa wao ni nyumba ya uasi. Wakati wa mchana, wakiwa wanakutazama, toa nje mizigo yako iliyofungwa kwa ajili ya kwenda uhamishoni. Kisha wakati wa jioni, wakiwa wanakutazama toka nje kama wale wanaoenda uhamishoni. Wakiwa wanakutazama, toboa ukuta utolee mizigo yako hapo. Beba mizigo hiyo begani mwako wakikuangalia uichukue nje wakati wa giza la jioni. Funika uso wako ili usione nchi, kwa maana nimekufanya ishara kwa nyumba ya Israeli.” Basi nikafanya kama nilivyoamriwa. Wakati wa mchana nilitoa vitu vyangu nje vilivyofungwa tayari kwa uhamishoni. Kisha wakati wa jioni nikatoboa ukuta kwa mikono yangu. Nikachukua mizigo yangu nje wakati wa giza la jioni, nikiwa nimeibeba mabegani mwangu huku wakinitazama. Asubuhi neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: “Mwanadamu, je, nyumba ile ya uasi ya Israeli haikukuuliza, ‘Unafanya nini?’ “Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Unabii huu unamhusu mkuu aliye katika Yerusalemu na watu wote wa nyumba ya Israeli walio huko.’ Waambie, ‘Mimi ni ishara kwenu.’ “Kama vile nilivyotenda, basi litatendeka vivyo hivyo kwao. Wataenda uhamishoni kama mateka. “Mkuu aliye miongoni mwao atabeba mizigo yake begani wakati wa giza la jioni na kuondoka, na tundu litatobolewa ukutani ili apite. Atafunika uso wake ili asiweze kuiona nchi. Nitamtandazia wavu wangu, naye atanaswa kwenye mtego wangu; nitamleta hadi Babeli, nchi ya Wakaldayo, lakini hataiona, naye atafia huko. Wote wanaomzunguka nitawatawanya pande zote: watumishi wake na majeshi yake yote; nami nitawafuatilia kwa upanga. “Wao watajua kwamba Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapowatawanya miongoni mwa mataifa, na kuwatapanya katika nchi zote. Lakini nitawaokoa wachache wao, wasiuawe kwa upanga, njaa na tauni, ili katika mataifa watakakoenda waweze kukiri matendo yao yote ya kuchukiza. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.”