Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 12

12
Uhamisho waelezewa kwa ishara
1Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 2“Mwanadamu, unaishi miongoni mwa watu waasi. Wana macho ya kuona, lakini hawaoni, na masikio ya kusikia lakini hawasikii, kwa kuwa ni watu waasi.
3“Kwa hiyo, mwanadamu, funga mizigo yako kwa kwenda uhamishoni tena wakati wa mchana, wakiwa wanakutazama, toka nje na uende mahali pengine kutoka hapo ulipo. Huenda wataelewa, ingawa wao ni nyumba ya uasi. 4Wakati wa mchana, wakiwa wanakutazama, toa nje mizigo yako iliyofungwa kwa ajili ya kwenda uhamishoni. Kisha wakati wa jioni, wakiwa wanakutazama toka nje kama wale wanaoenda uhamishoni. 5Wakiwa wanakutazama, toboa ukuta utolee mizigo yako hapo. 6Beba mizigo hiyo begani mwako wakikuangalia uichukue nje wakati wa giza la jioni. Funika uso wako ili usione nchi, kwa maana nimekufanya ishara kwa nyumba ya Israeli.”
7Basi nikafanya kama nilivyoamriwa. Wakati wa mchana nilitoa vitu vyangu nje vilivyofungwa tayari kwa uhamishoni. Kisha wakati wa jioni nikatoboa ukuta kwa mikono yangu. Nikachukua mizigo yangu nje wakati wa giza la jioni, nikiwa nimeibeba mabegani mwangu huku wakinitazama.
8Asubuhi neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 9“Mwanadamu, je, nyumba ile ya uasi ya Israeli haikukuuliza, ‘Unafanya nini?’
10“Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Unabii huu unamhusu mkuu aliye katika Yerusalemu na watu wote wa nyumba ya Israeli walio huko.’ 11Waambie, ‘Mimi ni ishara kwenu.’
“Kama vile nilivyotenda, basi litatendeka vivyo hivyo kwao. Wataenda uhamishoni kama mateka.
12“Mkuu aliye miongoni mwao atabeba mizigo yake begani wakati wa giza la jioni na kuondoka, na tundu litatobolewa ukutani ili apite. Atafunika uso wake ili asiweze kuiona nchi. 13Nitamtandazia wavu wangu, naye atanaswa kwenye mtego wangu; nitamleta hadi Babeli, nchi ya Wakaldayo, lakini hataiona, naye atafia huko. 14Wote wanaomzunguka nitawatawanya pande zote: watumishi wake na majeshi yake yote; nami nitawafuatilia kwa upanga.
15“Wao watajua kwamba Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapowatawanya miongoni mwa mataifa, na kuwatapanya katika nchi zote. 16Lakini nitawaokoa wachache wao, wasiuawe kwa upanga, njaa na tauni, ili katika mataifa watakakoenda waweze kukiri matendo yao yote ya kuchukiza. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.”
17Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 18“Mwanadamu, tetemeka unapokula chakula chako, tetemeka kwa hofu unapokunywa maji yako. 19Waambie watu wa nchi: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kuhusu wakaaji wa Yerusalemu na katika nchi ya Israeli: Watakula chakula chao kwa wasiwasi na kunywa maji yao kwa kufadhaika, kwa kuwa nchi yao itanyang’anywa kila kitu chake kwa sababu ya udhalimu wa wote wanaoishi humo. 20Miji inayokaliwa na watu itaharibiwa na nchi itakuwa ukiwa. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
21Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 22“Mwanadamu, ni ipi hii mithali mlio nayo katika nchi ya Israeli: ‘Siku zinapita na hakuna maono yoyote yanayotimia’? 23Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitaikomesha mithali hii, nao hawataitumia tena katika Israeli.’ Waambie, ‘Siku zimekaribia ambapo kila ono litatimizwa. 24Kwa maana hapatakuwa tena na maono ya uongo wala ubashiri wa kujipendekeza miongoni mwa watu wa Israeli. 25Lakini Mimi Mwenyezi Mungu nitasema neno nitakalo, nalo litatimizwa bila kuchelewa. Kwa kuwa katika siku zako, ewe nyumba ya uasi, nitatimiza kila nisemalo, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
26Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 27“Mwanadamu, nyumba ya Israeli inasema, ‘Maono yale anayoyaona ni kwa ajili ya miaka mingi ijayo, naye hutabiri kuhusu siku zijazo zilizo mbali.’
28“Kwa hiyo, waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Hakuna maneno yangu yatakayocheleweshwa tena zaidi, lolote nisemalo litatimizwa, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”

Iliyochaguliwa sasa

Ezekieli 12: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia