Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 13

13
Manabii wa uongo walaumiwa
1Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 2“Mwanadamu, tabiri dhidi ya manabii wa Israeli wanaotabiri sasa. Waambie hao ambao hutabiri kutokana na mawazo yao wenyewe: ‘Sikia neno la Mwenyezi Mungu! 3Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ole wao manabii wapumbavu wafuatao roho yao wenyewe na wala hawajaona chochote! 4Manabii wako, ee Israeli, ni kama mbweha katikati ya magofu. 5Hamjakwea kwenda kuziba mahali palipobomoka katika ukuta ili kuukarabati kwa ajili ya nyumba ya Israeli, ili isimame imara kwenye vita katika siku ya Mwenyezi Mungu. 6Maono yao ni ya uongo na ubashiri wao ni wa udanganyifu. Wao husema, “Mwenyezi Mungu amesema”, wakati Mwenyezi Mungu hakuwatuma; bado wakitarajia maneno yao kutimizwa. 7Je, hamjaona maono ya uongo na kusema ubashiri wa udanganyifu, hapo msemapo, “Mwenyezi Mungu asema”, wakati Mimi sijasema?
8“ ‘Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa sababu ya maneno yenu ya uongo na maono yenu ya udanganyifu, Mimi niko kinyume nanyi, asema Bwana Mungu Mwenyezi. 9Mkono wangu utakuwa dhidi ya manabii ambao huona maono ya uongo na kusema ubashiri wa udanganyifu. Hawatakuwa katika baraza la watu wangu au kuorodheshwa katika kumbukumbu ya nyumba ya Israeli, wala hawataingia katika nchi ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana Mungu Mwenyezi.
10“ ‘Kwa sababu wanapotosha watu wangu, wakisema, “Amani”, wakati hakuna amani; pia kwa sababu, wakati ukuta dhaifu unapojengwa, wanaufunika kwa kupaka chokaa, 11kwa hiyo waambie hao wanaoupaka chokaa isiyokorogwa vyema kwamba ukuta huo utaanguka. Mvua kubwa ya mafuriko itanyesha, nami nitaleta mvua ya mawe inyeshe kwa nguvu, nao upepo wa dhoruba utavuma juu yake. 12Ukuta utakapoanguka, je, watu hawatawauliza, “Iko wapi chokaa mliyopaka ukuta?”
13“ ‘Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Katika ghadhabu yangu nitauachia upepo wa dhoruba, na katika hasira yangu, mvua ya mawe na ya mafuriko itanyesha, ikiwa na ghadhabu ya kuangamiza. 14Nitaubomoa ukuta mlioupaka chokaa na kuuangusha chini ili msingi wake uwe wazi. Utakapoanguka, mtaangamizwa ndani yake, nanyi mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu. 15Hivyo ndivyo nitakavyoitimiza ghadhabu yangu dhidi ya huo ukuta na dhidi yao walioupaka chokaa. Nitawaambia ninyi, “Ukuta umebomoka na vivyo hivyo wale walioupaka chokaa, 16wale manabii wa Israeli walioitabiria Yerusalemu na kuona maono ya amani kwa ajili yake wakati hakukuwa na amani, asema Bwana Mungu Mwenyezi.” ’
17“Sasa, mwanadamu, kaza uso wako dhidi ya binti za watu wako wanaotabiri mambo kutoka mawazo yao wenyewe. Tabiri dhidi yao 18na useme, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ole wao wanawake washonao hirizi za uchawi juu ya viwiko vyao vyote na kutengeneza shela za urefu wa aina mbalimbali kwa ajili ya kufunika vichwa vyao kwa makusudi ya kuwanasa watu. Je, mtatega uhai wa watu wangu lakini ninyi mponye wa kwenu? 19Ninyi mmeninajisi miongoni mwa watu wangu kwa ajili ya konzi chache za shayiri na chembe za mkate. Kwa kuwanenea uongo watu wangu, ambao husikiliza uongo, mmewaua watu ambao hawakustahili kufa, na kuwaacha hai wale ambao walistahili kufa.
20“ ‘Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Niko kinyume na hizo hirizi zenu za uchawi mnazotumia kuwatega watu kama ndege, nami nitazirarua mikononi mwenu; nitawaweka huru watu mliowatega kama ndege. 21Nitazirarua shela zenu na kuwaokoa watu wangu kutoka mikononi mwenu, nao hawatakuwa tena mawindo ya nguvu zenu. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu. 22Kwa sababu mliwavunja moyo wenye haki kwa uongo wenu, wakati mimi sikuwaletea huzuni na kwa kuwa mliwatia moyo waovu ili wasiziache njia zao mbaya na hivyo kuokoa maisha yao, 23kwa hiyo hamtaona tena maono ya uongo wala kufanya ubashiri. Nitawaokoa watu wangu kutoka mikononi mwenu. Nanyi ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”

Iliyochaguliwa sasa

Ezekieli 13: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia