Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 14

14
Waabudu sanamu walaumiwa
1Baadhi ya wazee wa Israeli walinijia na kuketi mbele yangu. 2Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 3“Mwanadamu, watu hawa wameweka sanamu katika mioyo yao na kuweka vitu viovu vya kukwaza mbele ya macho yao. Je, kweli niwaruhusu waniulize jambo lolote? 4Kwa hiyo sema nao uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mwisraeli yeyote anapoweka sanamu moyoni mwake na kuweka kitu kiovu cha kukwaza mbele ya macho yake na kisha akaenda kwa nabii, Mimi Mwenyezi Mungu nitamjibu peke yangu sawasawa na ukubwa wa ibada yake ya sanamu. 5Nitafanya jambo hili ili kukamata tena mioyo ya watu wa Israeli, ambao wote wameniacha kwa ajili ya sanamu zao.’
6“Kwa hiyo iambie nyumba ya Israeli, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Tubuni! Acheni sanamu zenu, na matendo yenu yote ya machukizo!
7“ ‘Mwisraeli au mgeni yeyote anayeishi Israeli anapojitenga nami, na kujiwekea sanamu moyoni mwake, na hivyo kuweka kitu kiovu cha kukwaza mbele ya macho yake, na kisha akamwendea nabii kuuliza shauri kwangu, Mimi Mwenyezi Mungu nitamjibu mwenyewe. 8Nitamkabili mtu huyo na kumwadhibu, na kumfanya ishara na mithali. Nitamkatilia mbali kutoka kwa watu wangu. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
9“ ‘Na ikiwa nabii ameshawishika kutoa unabii, Mimi Mwenyezi Mungu nitakuwa nimemshawishi nabii huyo; nami nitaunyoosha mkono wangu dhidi yake na kumwangamiza kutoka miongoni mwa watu wangu Israeli. 10Watawajibika kwa hatia yao: nabii atakuwa na hatia sawa na yule mtu aliyekuja kuuliza neno kwake.
11“ ‘Ndipo watu wa Israeli hawataniacha tena, wala kujitia unajisi tena kwa dhambi zao zote. Watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
Hukumu isiyoepukika
12Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema, 13“Mwanadamu, nchi ikinitenda dhambi kwa kutokuwa waaminifu nami nikaunyoosha mkono wangu dhidi yake ili kukatilia mbali upatikanaji wake wa chakula na kuipelekea njaa na kuua watu wake na wanyama wao, 14hata kama watu hawa watatu: Nuhu, Danieli na Ayubu wangekuwa ndani ya nchi hiyo, wangeweza kujiokoa hao wenyewe tu kwa uadilifu wao, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
15“Au nikiwaachilia wanyama pori katika nchi hiyo nao wakaiacha bila watoto, nayo ikawa ukiwa hivi kwamba hakuna mtu apitaye kwa sababu ya wanyama pori, 16hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, hata kama watu hawa watatu wangekuwa ndani yake, wasingeweza kuokoa wana wao wala binti zao. Wao peke yao wangeokolewa, lakini nchi ingekuwa ukiwa.
17“Au nikileta upanga dhidi ya nchi hiyo na kusema, ‘Upanga na upite katika nchi yote,’ nami nikaua watu wa nchi hiyo na wanyama wao, 18hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, hata kama watu hawa watatu wangekuwa ndani yake, wasingeweza kuokoa wana wao wala binti zao. Wao wenyewe tu wangeokolewa.
19“Au nikipeleka tauni katika nchi hiyo na kumwaga ghadhabu yangu juu yake kupitia kumwaga damu, kuua watu wa nchi hiyo na wanyama wao, 20hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, hata kama Nuhu, Danieli na Ayubu wangekuwa ndani yake, wasingeweza kumwokoa mwana wala binti. Wao wangeweza kujiokoa wenyewe tu kwa uadilifu wao.
21“Kwa maana hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Itakuwa vibaya kiasi gani nitakapopeleka dhidi ya Yerusalemu hukumu zangu nne za kutisha, yaani upanga, njaa, wanyama pori na tauni, ili kuua watu wake na wanyama wao! 22Lakini patakuwa na watakaookoka: wana wa kiume na wa kike watakaoletwa kutoka nchi hiyo. Watakuja kwenu, nanyi mtakapoona mwenendo wao na matendo yao, mtafarijika kuhusu maafa niliyoleta juu ya Yerusalemu, kwa ajili ya maafa yale yote niliyoleta juu yake. 23Mtafarijika mtakapoona mwenendo wao na matendo yao, kwani mtajua kuwa sikufanya lolote ndani yake bila sababu, asema Bwana Mungu Mwenyezi.”

Iliyochaguliwa sasa

Ezekieli 14: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia