Ezekieli 16:15-34
Ezekieli 16:15-34 NENO
“ ‘Lakini ulitumainia uzuri wako na kutumia umaarufu wako kuwa kahaba. Ulifanya uasherati na kila mtu aliyepita, nao uzuri wako ukawa wake. Ulichukua baadhi ya mavazi yako, ukayatumia kupamba mahali pako pa juu pa kuabudia, ambapo uliendeleza ukahaba wako. Mambo kama hayo hayastahili kutendeka wala kamwe kufanyika. Pia ulichukua vito vizuri nilivyokupa, vito vilivyotengenezwa kwa dhahabu yangu na fedha yangu, ukajitengenezea navyo sanamu za kiume na ukafanya ukahaba nazo. Ukayachukua mavazi yako yaliyotariziwa, na kuyavalisha hizo sanamu, ukatoa mbele ya hizo sanamu mafuta yangu na uvumba wangu. Pia chakula changu nilichokupa ili ule: unga laini, mafuta ya zeituni na asali, ulivitoa mbele yao kuwa uvumba wa harufu nzuri. Hayo ndiyo yaliyotokea, asema Bwana Mungu Mwenyezi. “ ‘Nawe uliwachukua wanao wa kiume na wa kike ulionizalia na kuwatoa kafara kuwa chakula kwa sanamu. Je, ukahaba wako haukukutosha? Uliwachinja watoto wangu na kuwatoa kafara kwa sanamu. Katika matendo yako yote ya machukizo pamoja na ukahaba wako, hukukumbuka siku za ujana wako, wakati ulipokuwa uchi kabisa bila kitu chochote, ulipokuwa ukigaagaa kwenye damu yako. “ ‘Ole! Ole wako! Asema Bwana Mungu Mwenyezi. Pamoja na maovu yako yote mengine, Ulijijengea jukwaa na kujifanyia mahali pa fahari pa ibada za sanamu kwenye kila uwanja wa mikutano. Katika kila mwanzo wa barabara ulijenga mahali pa fahari pa ibada za sanamu, na kuuaibisha uzuri wako, ukizidi kuutoa mwili wako kwa uzinzi kwa kila apitaye. Ulifanya ukahaba wako na Wamisri, majirani zako waliojaa tamaa, ukaichochea hasira yangu kwa kuongezeka kwa uzinzi wako. Hivyo niliunyoosha mkono wangu dhidi yako na kuipunguza nchi yako; nikakutia kwenye ulafi wa adui zako, binti za Wafilisti, walioshtushwa na tabia yako ya uasherati. Ulifanya ukahaba na Waashuru pia, kwa kuwa hukuridhika, hata baada ya hayo, ukawa bado hukutosheleka. Ndipo uliuzidisha uzinzi wako kwa kujumuisha Ukaldayo, nchi ya wafanyabiashara; lakini hata katika hili hukutosheka. “ ‘Tazama jinsi ulivyo na dhamiri dhaifu, asema Bwana Mungu Mwenyezi, unapofanya mambo haya yote, unatenda kama kahaba asiye aibu! Ulipojenga jukwaa lako katika mwanzo wa kila barabara, na kutengeneza mahali pako pa fahari pa ibada za sanamu katika kila kiwanja cha wazi, hukuwa kama kahaba, kwa sababu ulidharau malipo. “ ‘Wewe mke mzinzi! Unapenda wageni, kuliko mume wako mwenyewe. Kila kahaba hupokea malipo, lakini wewe hutoa zawadi kwa wapenzi wako wote, ukiwahonga ili waje kwako kutoka kila mahali kwa ajili ya ukahaba wako. Kwa hiyo wewe ulikuwa tofauti na wanawake wengine kwenye ukahaba wako. Hakuna aliyekutongoza ili kuzini naye, bali wewe ulikuwa tofauti kabisa, kwani ulilipa wakati hakuna malipo uliyolipwa wewe.