Ezekieli 16:35-43
Ezekieli 16:35-43 NENO
“ ‘Kwa hiyo, wewe kahaba, sikia neno la Mwenyezi Mungu! Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa kuwa umemwaga tamaa zako na kuonesha uchi wako katika uzinzi wako kwa wapenzi wako na kwa sababu ya sanamu zako zote za machukizo na kwa sababu uliwapa damu ya watoto wako, kwa hiyo nitawakusanya wapenzi wako wote, wale uliojifurahisha nao: wale uliowapenda kadhalika na wale uliowachukia. Nitawakusanya wote dhidi yako kutoka pande zote, na nitakuvua nguo mbele yao, nao wataona uchi wako wote. Nitakuhukumia adhabu wanayopewa wanawake wafanyao uasherati na hao wanaomwaga damu; nitaleta juu yako kisasi cha damu cha ghadhabu yangu na hasira yangu yenye wivu. Kisha nitakutia mikononi mwa wapenzi wako, nao watabomoa majukwaa yako na kuharibu mahali pako pa fahari pa ibada za sanamu. Watakuvua nguo zako na kuchukua vito vyako vya thamani na kukuacha uchi na bila kitu. Wataleta kundi la watu dhidi yako, watakaokupiga kwa mawe na kukukatakata vipande vipande kwa panga zao. Watachoma nyumba zako na kutekeleza adhabu juu yako machoni pa wanawake wengi. Nitakomesha ukahaba wako, nawe hutawalipa tena wapenzi wako. Ndipo ghadhabu yangu dhidi yako itapungua, na hasira yangu yenye wivu itakuondokea. Nitatulia, wala sitakasirika tena. “ ‘Kwa sababu hukuzikumbuka siku za ujana wako, lakini ulinighadhibisha kwa mambo haya yote, hakika nitaleta juu ya kichwa chako yale uliyotenda, asema Bwana Mungu Mwenyezi. Je, hukuongeza uasherati juu ya matendo yako mengine ya kuchukiza?