Ezekieli 17
17
Tai wawili na mizabibu
1Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 2“Mwanadamu, tega kitendawili, ukawaambie nyumba ya Israeli fumbo. 3Waambie hivi, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Tai mkubwa mwenye mabawa yenye nguvu, yaliyojaa manyoya marefu ya rangi mbalimbali, alikuja Lebanoni. Akatua kwenye kilele cha mwerezi, 4akakwanyua ncha yake na kuichukua hadi nchi ya wafanyabiashara, akaipanda huko katika mji wa wachuuzi.
5“ ‘Akachukua baadhi ya mbegu za nchi yako na kuziweka katika udongo wenye rutuba. Akazipanda kama mti umeao kando ya maji mengi, 6nazo zikaota na kuwa mzabibu mfupi, unaoeneza matawi yake. Matawi yake yakamwelekea huyo tai, mizizi yake ikabaki chini ya huo mzabibu. Kwa hiyo ukawa mzabibu na kutoa matawi na vitawi vyenye majani mengi.
7“ ‘Lakini kulikuwa na tai mwingine mkubwa, mwenye mabawa yenye nguvu yaliyojaa manyoya. Tazama! Huu mzabibu ukatoa mizizi yake kumwelekea huyo tai kutoka mle kwenye shamba lile ulikopandwa, na kutanda matawi yake kumwelekea ili aunyweshe maji. 8Ulikuwa umepandwa katika udongo mzuri wenye maji mengi ili uweze kutoa matawi, kuzaa matunda, na uweze kuwa mzabibu mzuri sana.’
9“Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Je, utastawi? Je, hautang’olewa na kuondolewa matunda yake, ili uweze kunyauka? Majani yake mapya yanayochipua yote yatanyauka. Hautahitaji mkono wenye nguvu au watu wengi kuung’oa na mizizi yake. 10Hata kama utapandwa pengine, je, utastawi? Je, hautanyauka kabisa wakati upepo wa mashariki utakapoupiga, yaani hautanyauka kabisa katika udongo mzuri ambamo ulikuwa umestawi vizuri?’ ”
11Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 12“Waambie nyumba hii ya uasi, ‘Je, mnajua hii ina maana gani?’ Waambie: ‘Mfalme wa Babeli alienda Yerusalemu na kumchukua mfalme wake na watu wake maarufu, akawaleta Babeli. 13Ndipo akamchukua mmoja wa jamaa ya mfalme na kufanya mapatano naye, akamfanya aape. Akawachukua pia viongozi wa nchi, 14ili kuudhoofisha ufalme huo, usiweze kuinuka tena, ila uweze kuendelea tu chini ya mapatano yake. 15Lakini mfalme aliasi dhidi yake kwa kutuma wajumbe wake kwenda Misri ili kupatiwa farasi na jeshi kubwa. Je, atashinda? Je, atafanikiwa? Je, mtu afanyaye mambo kama hayo ataokoka? Je, atavunja mapatano na bado aokoke?
16“ ‘Hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, atafia huko Babeli, katika nchi ya mfalme aliyemketisha kwenye kiti cha utawala, ambaye alidharau kiapo chake na kuvunja mapatano yake. 17Farao pamoja na jeshi lake kubwa na watu wake wengi hawataweza kusaidia chochote katika vita, watakapozingirwa na jeshi likitaka kuangamiza watu wengi. 18Alidharau kiapo kwa kulivunja agano. Kwa sababu aliahidi kwa mkono wake mwenyewe na bado akafanya mambo haya yote, hataokoka.
19“ ‘Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Hakika kama niishivyo, nitamwadhibu kwa kudharau kiapo changu, na kulivunja agano langu. 20Nitautandaza wavu wangu kwa ajili yake, naye atanaswa katika mtego wangu. Nitamleta Babeli na kutekeleza hukumu juu yake huko kwa kuwa hakuwa mwaminifu kwangu. 21Askari wake wote wanaotoroka wataanguka kwa upanga, nao watakaonusurika watatawanyika katika pande zote za dunia. Ndipo utakapojua kuwa Mimi Mwenyezi Mungu nimesema.
Hatimaye Israeli kutukuzwa
22“ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mimi mwenyewe nitachukua chipukizi kutoka kilele cha juu sana cha mwerezi na kukipanda, nitavunja kitawi kichanga kutoka matawi yake ya juu kabisa na kukipanda juu ya mlima mrefu ulioinuka sana. 23Katika vilele vya mlima mrefu wa Israeli nitakipanda, kitatoa matawi na kuzaa matunda na kuwa mwerezi mzuri sana. Ndege wa kila aina watajenga viota vyao ndani yake, nao watapata makazi katika kivuli cha matawi yake. 24Miti yote ya kondeni itajua kuwa Mimi Mwenyezi Mungu ninaishusha miti mirefu na kuikuza miti mifupi kuwa miti mirefu. Mimi naikausha miti mibichi na kuifanya miti mikavu istawi.
“ ‘Mimi Mwenyezi Mungu nimesema, nami nitatenda.’ ”
Iliyochaguliwa sasa
Ezekieli 17: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.