Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 23:36-49

Ezekieli 23:36-49 NEN

BWANA akaniambia, “Mwanadamu, Je, utawahukumu Ohola na Oholiba? Basi wakabili kwa ajili ya matendo yao ya machukizo, kwa kuwa wamefanya uzinzi na damu imo mikononi mwao. Wamefanya uzinzi na sanamu zao, hata wamewatoa watoto wao walionizalia kuwa kafara, kuwa chakula kwao. Pia wamenifanyia hili: wakati huo huo wamenajisi patakatifu pangu na kuzitangua Sabato zangu. Siku ile ile walitoa watoto wao kuwa kafara kwa sanamu zao, waliingia patakatifu pangu na kupatia unajisi. Hilo ndilo walilolifanya katika nyumba yangu. “Walituma hata wajumbe kuwaita watu kutoka mbali, nao walipowasili ulioga kwa ajili yao, ukapaka macho yako rangi na ukavaa mapambo yako yaliyotengenezwa kwa vito vya dhahabu. Ukaketi kwenye kiti cha anasa, kukiwa na meza iliyoandaliwa mbele yake ambayo juu yake ulikuwa umeweka uvumba na mafuta ambayo yalikuwa yangu. “Kelele za umati wa watu wasiojali zilikuwa zimemzunguka, wakaleta watu wengi waliokuwa wakifanya makelele na walevi kutoka nyikani, ambao walitia bangili kwenye mikono ya yule mwanamke na dada yake na pia taji nzuri za kupendeza kwenye vichwa vyao. Ndipo nikasema kuhusu yule aliyechakazwa na uzinzi, ‘Basi wamtumie kama kahaba, kwa kuwa ndivyo alivyo.’ Nao wakazini naye. Kama vile watu wazinivyo na kahaba, ndiyo hivyo walivyozini na hao wanawake waasherati, Ohola na Oholiba. Lakini watu wenye haki, watawahukumia adhabu wanawake wafanyao uzinzi na kumwaga damu, kwa kuwa ni wazinzi na damu iko mikononi mwao. “Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo, Leteni watu wengi wenye makelele dhidi yao na uwaache wapate hofu na watekwe nyara. Hao watu wengi watawapiga kwa mawe na kuwaua kwa panga zao, watawaua wana wao na binti zao na kuzichoma nyumba zao. “Hivyo nitaukomesha uasherati katika nchi, ili wanawake wote wapate onyo nao wasije wakafanya uasherati kama ninyi mlivyofanya. Utapata adhabu kwa ajili ya uasherati wako na kuchukua matokeo ya dhambi zako za uasherati. Ndipo utakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA Mwenyezi.”