Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 23:36-49

Ezekieli 23:36-49 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwenyezi-Mungu aliniambia, “Wewe mtu! Je, uko tayari kuwahukumu Ohola na Oholiba? Basi, watangazie matendo yao ya kuchukiza! Wamefanya uzinzi na mauaji. Wamefanya ukahaba kwa sanamu zao, hata kuzitambikia watoto walionizalia wao wenyewe. Tena si hayo tu! Wameikufuru maskani yangu na kuzitangua sabato zangu. Siku ileile walipozitambikia sanamu watoto wao wenyewe, waliingia patakatifu ili wapatie unajisi. Hayo ndiyo waliyoyafanya nyumbani mwangu. “Hata walituma wajumbe wawaite watu wa mbali, nao wakaja. Kwa ajili yao, walioga, wakajitia wanja na kujipamba kwa johari. Kisha wakawa wameketi kwenye makochi mazurimazuri, na mbele yao meza imetandikwa. Juu ya meza hiyo waliweka ubani wangu na mafuta yangu. Basi, kukasikika sauti za kundi la watu wasiojali kitu, kundi la wanaume walevi walioletwa kutoka jangwani. Waliwavisha hao wanawake bangili mikononi mwao na taji nzuri vichwani mwao. Ndipo nikasema: Wanazini na mwanamke aliyechakaa kwa uzinzi. Kila mmoja alimwendea kama wanaume wamwendeavyo malaya. Ndivyo walivyowaendea Ohola na Oholiba wale wanawake waasherati. Lakini waamuzi waadilifu watawahukumu jinsi wanavyohukumu wazinzi na wauaji; kwa maana ni wazinzi na wauaji. “Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Genge la watu litaletwa, litawatisha na kuwapora mali zao. Genge hilo la watu litawapiga mawe, litawashambulia kwa upanga na kuwaua wana wao na binti zao, na nyumba zao wataziteketeza kwa moto. Ndivyo nitakavyokomesha uasherati wao katika nchi nzima, liwe onyo kwa wanawake wote wasifanye uzinzi kama huo mlioufanya. Na nyinyi Ohola na Oholiba, mtaadhibiwa kutokana na uzinzi wenu na dhambi yenu ya kuziabudu sanamu za miungu. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Bwana Mwenyezi-Mungu.”

Ezekieli 23:36-49 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Tena BWANA akaniambia, Mwanadamu, utawahukumu Ohola na Oholiba? Basi watangazie matendo yao maovu. Maana wamezini, na damu imo mikononi mwao, nao wamezini na vinyago vyao; tena wana wao walionizalia wamewapitisha katika moto ili waliwe nao. Tena wamenitenda haya; wamepatia unajisi mahali pangu patakatifu, siku ile ile, nao wamezitangua sabato zangu. Kwa maana walipokuwa wamekwisha kuvichinjia vinyago vyao watoto wao, ndipo walipoingia patakatifu pangu, siku ile ile, wapatie unajisi, na tazama, wamefanya hivyo katika nyumba yangu. Tena mmewatuma watu kuwaita watokao mbali; ambao mjumbe alitumwa kwao, na tazama, wakaja; nawe ulijiosha kwa ajili yao, ulitia rangi macho yako, na kuremba kwa mapambo mazuri; ukaketi juu ya kitanda cha enzi, na meza imeandikwa tayari mbele yake, ambayo juu yake uliweka uvumba wangu na mafuta yangu. Na sauti za wingi wa watu wenye hali ya raha zilikuwa pamoja naye; na pamoja na watu wasio na adabu, waliletwa walevi toka jangwani; wakawatia vikuku mikononi, na taji zuri juu ya vichwa vyao. Ndipo nikasema, Huyo aliye mkongwe atafanya uzinzi! Sasa hao watazini naye, naam, na yeye! Wakamwingilia kama watu wamwingiliavyo kahaba; ndivyo walivyowaingilia Ohola na Oholiba, wanawake wale waasherati. Basi watu wenye haki watawahukumu, kwa hukumu iwapasayo wazinzi, na kwa hukumu iwapasayo wanawake wamwagao damu; kwa sababu wao ndio wazinzi, na mikononi mwao mna damu. Maana Bwana MUNGU asema hivi; Nitaleta kusanyiko la watu juu yao, nami nitawatoa warushwe huku na huko, na kutekwa nyara. Na kusanyiko hilo watawapiga kwa mawe, na kuwaua kwa panga zao; watawaua wana wao na binti zao, na kuziteketeza nyumba zao kwa moto. Hivyo nitaukomesha uasherati katika nchi hii, ili wanawake wote wafundishwe, wasifanye uasherati kama mlivyofanya. Nao watawalipa ninyi malipo ya uasherati wenu, nanyi mtachukua dhambi za vinyago vyenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU.

Ezekieli 23:36-49 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Tena BWANA akaniambia, Mwanadamu, utawahukumu Ohola na Oholiba? Basi uwahubiri machukizo yao. Maana wamezini, na damu imo mikononi mwao, nao wamezini na vinyago vyao; tena wana wao walionizalia wamewapitisha katika moto ili waliwe nao. Tena wamenitenda haya; wamepatia unajisi mahali pangu patakatifu, siku ile ile, nao wamezitangua sabato zangu. Kwa maana walipokuwa wamekwisha kuvichinjia vinyago vyao watoto wao, ndipo walipoingia patakatifu pangu, siku ile ile, wapatie unajisi, na tazama, wamefanya hivyo kati ya nyumba yangu. Tena mmewatuma watu kuwaita watokao mbali; ambao mjumbe alitumwa kwao, na tazama, wakaja; nawe ulijiosha kwa ajili yao, ulitia rangi macho yako, na kujipamba vyombo vya uzuri; ukaketi juu ya kitanda cha enzi, na meza imeandikwa tayari mbele yake, ambayo juu yake uliweka uvumba wangu na mafuta yangu. Na sauti za wingi wa watu wenye hali ya raha zilikuwa pamoja naye; na pamoja na watu wasio na adabu, waliletwa walevi toka jangwani; wakawatia vikuku mikononi, na taji nzuri juu ya vichwa vyao. Ndipo nikasema, Huyo aliye mkongwe atafanya uzinzi! Sasa hao watazini naye, naam, na yeye! Wakamwingilia kama watu wamwingiliavyo kahaba; ndivyo walivyowaingilia Ohola na Oholiba, wanawake wale waasherati. Basi watu wenye haki watawahukumu, kwa hukumu iwapasayo wazinzi, na kwa hukumu iwapasayo wanawake wamwagao damu; kwa sababu wao ndio wazinzi, na mikononi mwao mna damu. Maana Bwana MUNGU asema hivi; Nitaleta kusanyiko la watu juu yao, nami nitawatoa warushwe huko na huko, na kutekwa nyara. Na kusanyiko hilo watawapiga kwa mawe, na kuwaua kwa panga zao; watawaua wana wao na binti zao, na kuziteketeza nyumba zao kwa moto. Hivyo nitaukomesha uasherati katika nchi hii, ili wanawake wote wafundishwe, wasifanye mambo ya uasherati wenu. Nao watawalipa ninyi malipo ya uasherati wenu, nanyi mtachukua dhambi za vinyago vyenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU.

Ezekieli 23:36-49 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

BWANA akaniambia, “Mwanadamu, Je, utawahukumu Ohola na Oholiba? Basi wakabili kwa ajili ya matendo yao ya machukizo, kwa kuwa wamefanya uzinzi na damu imo mikononi mwao. Wamefanya uzinzi na sanamu zao, hata wamewatoa watoto wao walionizalia kuwa kafara, kuwa chakula kwao. Pia wamenifanyia hili: wakati huo huo wamenajisi patakatifu pangu na kuzitangua Sabato zangu. Siku ile ile walitoa watoto wao kuwa kafara kwa sanamu zao, waliingia patakatifu pangu na kupatia unajisi. Hilo ndilo walilolifanya katika nyumba yangu. “Walituma hata wajumbe kuwaita watu kutoka mbali, nao walipowasili ulioga kwa ajili yao, ukapaka macho yako rangi na ukavaa mapambo yako yaliyotengenezwa kwa vito vya dhahabu. Ukaketi kwenye kiti cha anasa, kukiwa na meza iliyoandaliwa mbele yake ambayo juu yake ulikuwa umeweka uvumba na mafuta ambayo yalikuwa yangu. “Kelele za umati wa watu wasiojali zilikuwa zimemzunguka, wakaleta watu wengi waliokuwa wakifanya makelele na walevi kutoka nyikani, ambao walitia bangili kwenye mikono ya yule mwanamke na dada yake na pia taji nzuri za kupendeza kwenye vichwa vyao. Ndipo nikasema kuhusu yule aliyechakazwa na uzinzi, ‘Basi wamtumie kama kahaba, kwa kuwa ndivyo alivyo.’ Nao wakazini naye. Kama vile watu wazinivyo na kahaba, ndiyo hivyo walivyozini na hao wanawake waasherati, Ohola na Oholiba. Lakini watu wenye haki, watawahukumia adhabu wanawake wafanyao uzinzi na kumwaga damu, kwa kuwa ni wazinzi na damu iko mikononi mwao. “Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo, Leteni watu wengi wenye makelele dhidi yao na uwaache wapate hofu na watekwe nyara. Hao watu wengi watawapiga kwa mawe na kuwaua kwa panga zao, watawaua wana wao na binti zao na kuzichoma nyumba zao. “Hivyo nitaukomesha uasherati katika nchi, ili wanawake wote wapate onyo nao wasije wakafanya uasherati kama ninyi mlivyofanya. Utapata adhabu kwa ajili ya uasherati wako na kuchukua matokeo ya dhambi zako za uasherati. Ndipo utakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA Mwenyezi.”