Ezekieli 23:36-49
Ezekieli 23:36-49 BHN
Mwenyezi-Mungu aliniambia, “Wewe mtu! Je, uko tayari kuwahukumu Ohola na Oholiba? Basi, watangazie matendo yao ya kuchukiza! Wamefanya uzinzi na mauaji. Wamefanya ukahaba kwa sanamu zao, hata kuzitambikia watoto walionizalia wao wenyewe. Tena si hayo tu! Wameikufuru maskani yangu na kuzitangua sabato zangu. Siku ileile walipozitambikia sanamu watoto wao wenyewe, waliingia patakatifu ili wapatie unajisi. Hayo ndiyo waliyoyafanya nyumbani mwangu. “Hata walituma wajumbe wawaite watu wa mbali, nao wakaja. Kwa ajili yao, walioga, wakajitia wanja na kujipamba kwa johari. Kisha wakawa wameketi kwenye makochi mazurimazuri, na mbele yao meza imetandikwa. Juu ya meza hiyo waliweka ubani wangu na mafuta yangu. Basi, kukasikika sauti za kundi la watu wasiojali kitu, kundi la wanaume walevi walioletwa kutoka jangwani. Waliwavisha hao wanawake bangili mikononi mwao na taji nzuri vichwani mwao. Ndipo nikasema: Wanazini na mwanamke aliyechakaa kwa uzinzi. Kila mmoja alimwendea kama wanaume wamwendeavyo malaya. Ndivyo walivyowaendea Ohola na Oholiba wale wanawake waasherati. Lakini waamuzi waadilifu watawahukumu jinsi wanavyohukumu wazinzi na wauaji; kwa maana ni wazinzi na wauaji. “Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Genge la watu litaletwa, litawatisha na kuwapora mali zao. Genge hilo la watu litawapiga mawe, litawashambulia kwa upanga na kuwaua wana wao na binti zao, na nyumba zao wataziteketeza kwa moto. Ndivyo nitakavyokomesha uasherati wao katika nchi nzima, liwe onyo kwa wanawake wote wasifanye uzinzi kama huo mlioufanya. Na nyinyi Ohola na Oholiba, mtaadhibiwa kutokana na uzinzi wenu na dhambi yenu ya kuziabudu sanamu za miungu. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Bwana Mwenyezi-Mungu.”