Ezekieli 28
28
Unabii Dhidi Ya Mfalme Wa Tiro
1Neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, mwambie mfalme wa Tiro, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:
“ ‘Kwa sababu moyo wako umejivuna
na umesema, “Mimi ni mungu;
nami ninaketi katika kiti cha enzi cha mungu
katika moyo wa bahari.”
Lakini wewe ni mwanadamu, wala si mungu,
ingawa unafikiri kuwa una hekima kama mungu.
3 Je, wewe una hekima kuliko Danieli?
Je, hakuna siri iliyofichika kwako?
4 Kwa hekima yako na ufahamu wako,
umejipatia utajiri,
nawe umejikusanyia dhahabu
na fedha katika hazina zako.
5 Kwa werevu wako mwingi katika biashara,
umeongeza utajiri wako
na kwa sababu ya utajiri wako
moyo wako umekuwa na kiburi.
6“ ‘Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:
“ ‘Kwa sababu unafikiri una hekima,
mwenye hekima kama mungu,
7 mimi nitawaleta wageni dhidi yako,
taifa katili kuliko yote;
watafuta panga zao dhidi ya uzuri wa hekima yako,
na kuchafua fahari yako inayongʼaa.
8 Watakushusha chini shimoni,
nawe utakufa kifo cha kikatili
katika moyo wa bahari.
9 Je, wakati huo utasema, “Mimi ni mungu,”
mbele ya wale wanaokuua?
Utakuwa mwanadamu tu, wala si mungu,
mikononi mwa hao wanaokuua.
10 Utakufa kifo cha wasiotahiriwa
kwa mkono wa wageni.
Kwa kuwa mimi nimenena, asema Bwana Mwenyezi.’ ”
11Neno la Bwana likanijia kusema: 12 “Mwanadamu, mfanyie maombolezo mfalme wa Tiro, nawe umwambie: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:
“ ‘Ulikuwa kipeo cha ukamilifu,
ukiwa umejaa hekima
na mkamilifu katika uzuri.
13 Ulikuwa ndani ya Edeni,
bustani ya Mungu;
kila kito cha thamani kilikupamba:
akiki nyekundu, yakuti manjano na zumaridi,
krisolitho, shohamu na yaspi,
yakuti samawi, almasi na zabarajadi.
Kuwekwa kwa hayo mapambo na kushikizwa kwake
kulifanywa kwa dhahabu;
siku ile ulipoumbwa yaliandaliwa tayari.
14 Ulitiwa mafuta kuwa kerubi mlinzi,
kwa kuwa hivyo ndivyo nilivyokuweka wakfu.
Ulikuwa kwenye mlima mtakatifu wa Mungu;
ulitembea katikati ya vito vya moto.
15Ulikuwa mnyofu katika njia zako
tangu siku ile ya kuumbwa kwako,
hadi uovu ulipoonekana ndani yako.
16 Kutokana na biashara yako iliyoenea,
ulijazwa na dhuluma,
nawe ukatenda dhambi.
Hivyo nilikuondoa kwa aibu kutoka mlima wa Mungu,
nami nikakufukuza, ee kerubi mlinzi,
kutoka katikati ya vito vya moto.
17 Moyo wako ukawa na kiburi
kwa ajili ya uzuri wako,
nawe ukaiharibu hekima yako
kwa sababu ya fahari yako.
Kwa hiyo nikakutupa chini;
nimekufanya kioja mbele ya wafalme.
18 Kwa dhambi zako nyingi na biashara yako ya dhuluma,
umenajisi mahali pako patakatifu.
Kwa hiyo nilifanya moto utoke ndani yako,
nao ukakuteketeza,
nami nikakufanya majivu juu ya nchi,
machoni pa wote waliokuwa wakitazama.
19 Mataifa yote yaliyokujua
yanakustajabia;
umefikia mwisho wa kutisha
na hutakuwepo tena milele.’ ”
Unabii Dhidi Ya Sidoni
20Neno la Bwana likanijia kusema: 21 “Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Sidoni, ukatabiri dhidi yake, 22 nawe useme: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:
“ ‘Mimi ni kinyume chako, ee Sidoni,
nami nitapata utukufu ndani yako.
Nao watajua kwamba Mimi ndimi Bwana,
nitakapotekeleza hukumu zangu
na kuonyesha utakatifu wangu ndani yake.
23 Nitapeleka tauni ndani yake
na kufanya damu itiririke katika barabara zake.
Waliochinjwa wataanguka ndani yake,
kwa upanga dhidi yake kila upande.
Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana.
24 “ ‘Nyumba ya Israeli hawatakuwa tena na majirani wenye nia ya kuwadhuru wanaoumiza kama michongoma na miiba mikali. Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana Mwenyezi.
25 “ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitakapoikusanya nyumba ya Israeli kutoka mataifa ambako wametawanyika, nitajionyesha kuwa mtakatifu miongoni mwao machoni pa mataifa. Ndipo watakapoishi katika nchi yao wenyewe, niliyompa mtumishi wangu Yakobo. 26 Wataishi humo kwa salama na watajenga nyumba na kupanda mashamba ya mizabibu, wataishi kwa salama nitakapowaadhibu majirani zao wote ambao waliwafanyia uovu. Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana, Mungu wao.’ ”
Iliyochaguliwa sasa
Ezekieli 28: NEN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.