Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 3:16-27

Ezekieli 3:16-27 NEN

Mwishoni mwa hizo siku saba neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, nimekufanya uwe mlinzi wa nyumba ya Israeli, kwa hiyo sikia neno nisemalo, ukawape onyo litokalo kwangu. Nimwambiapo mtu mwovu, ‘Hakika utakufa,’ na wewe usipomwonya mtu huyo au kumshauri aache njia zake mbaya ili kuokoa maisha yake, huyo mtu mwovu atakufa katika dhambi yake na damu yake nitaidai mkononi mwako. Lakini ukimwonya mtu mwovu naye akakataa kuacha uovu wake na njia zake mbaya, atakufa katika dhambi yake, lakini wewe utakuwa umejiokoa nafsi yako. “Tena, mtu mwenye haki akiacha haki yake na kutenda maovu, nami nikaweka kikwazo mbele yake mtu huyo atakufa. Kwa kuwa hukumwonya, atakufa katika dhambi yake. Mambo ya haki aliyotenda, hayatakumbukwa, damu yake nitaidai mkononi mwako. Lakini ukimwonya mwenye haki asitende dhambi na akaacha kutenda dhambi, hakika ataishi kwa sababu alipokea maonyo na utakuwa umejiokoa nafsi yako.” Mkono wa BWANA ulikuwa juu yangu huko, naye akaniambia, “Simama uende mpaka sehemu tambarare, nami nitasema nawe huko.” Kwa hiyo niliinuka nikaenda mpaka mahali pa tambarare. Utukufu wa BWANA ulikuwa umesimama huko, kama utukufu ule niliouona kando ya Mto Kebari, nami nikaanguka kifudifudi. Ndipo Roho akaja ndani yangu akanisimamisha kwa miguu yangu. Akasema nami akaniambia: “Nenda ukajifungie ndani ya nyumba yako. Nawe, ee mwanadamu, watakufunga kwa kamba, watakufunga ili usiweze kutoka na kuwaendea watu. Nitaufanya ulimi wako ushikamane kwenye kaa la kinywa chako, ili uwe kimya usiweze kuwakemea, wajapokuwa ni nyumba ya kuasi. Lakini nitakaposema nawe, nitafungua kinywa chako nawe utawaambia, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo.’ Yeyote atakayesikiliza na asikilize, na yeyote atakayekataa na akatae; kwa kuwa wao ni nyumba ya kuasi.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Ezekieli 3:16-27