Ezekieli 31
31
Farao, mwerezi ulioanguka
1Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa tatu, siku ya kwanza, neno la Mwenyezi Mungu likanijia, kusema: 2“Mwanadamu, mwambie Farao mfalme wa Misri na makundi yake hivi:
“ ‘Je, ni nani awezaye kulinganishwa
na wewe katika fahari.
3Angalia Ashuru, zamani ulikuwa mwerezi huko Lebanoni,
ukiwa na matawi mazuri
na kutia msitu kivuli;
ulikuwa mrefu sana, kilele chake
kilipita majani ya miti yote.
4Maji mengi yaliustawisha,
chemchemi zenye maji mengi
ziliufanya urefuke;
vijito vyake vilitiririka pale
ulipoota pande zote
na kupeleka mifereji yake
kwenye miti yote ya shambani.
5Hivyo ukarefuka
kupita miti yote ya shambani;
vitawi vyake viliongezeka
na matawi yake yakawa marefu,
yakitanda kwa sababu ya wingi wa maji.
6Ndege wote wa angani
wakaweka viota kwenye vitawi vyake,
wanyama wote wa shambani
wakazaana chini ya matawi yake,
mataifa makubwa yote
yaliishi chini ya kivuli chake.
7Ulikuwa na fahari katika uzuri,
ukiwa na matawi yaliyotanda,
kwa kuwa mizizi yake iliteremka
hadi kwenye maji mengi.
8Mierezi katika bustani ya Mungu
haikuweza kushindana nao,
wala misunobari haikuweza
kulingana na vitawi vyake,
wala miaramoni
haikulinganishwa na matawi yake,
wala hakukuwa na mti katika bustani ya Mungu
wa kulinganisha na uzuri wake.
9Niliufanya kuwa mzuri,
ukiwa na matawi mengi;
nao ulionewa wivu na miti yote ya Edeni
katika bustani ya Mungu.
10“ ‘Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa sababu ulikuwa mrefu sana, kilele chake kikiwa juu ya majani manene ya miti na kwa sababu ulikuwa na kiburi cha urefu wake, 11niliutia mikononi mwa mtawala wa mataifa, ili yeye autende sawasawa na uovu wake. Nikaukatilia mbali, 12nayo mataifa mageni yaliyo makatili sana yaliukata huo mti na kuuacha. Matawi yake yalianguka juu ya milima na kwenye mabonde yote, vitawi vyake vikavunjika na kusambaa katika makorongo yote ya nchi. Mataifa yote ya duniani yakaondoka kutoka kivuli chake na kuuacha. 13Ndege wote wa angani wakakaa kwenye ule mti ulioanguka na wanyama pori wote wakakaa katikati ya vitawi vyake. 14Kamwe hakutakuwa na miti mingine kando ya hayo maji itakayorefuka zaidi ya huo, vilele vyake vikiwa juu ya majani yote ya miti. Hakuna miti mingine, hata kama imekunywa maji vizuri namna gani, itakayofikia urefu huo. Yote mwisho wake ni kifo, na kuingia ardhini, kama vile ilivyo kwa wanadamu, pamoja na wale wanaoshuka shimoni.
15“ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Katika siku ile mwerezi uliposhushwa chini kaburini#31:15 Kaburini maana yake ni Kuzimu; kwa Kiebrania ni Sheol; pia 31:16, 17. nilizifunika chemchemi zenye maji mengi kwa maombolezo: Nilivizuia vijito vyake na wingi wa maji yake nikauzuia. Kwa sababu yake niliivika Lebanoni huzuni, nayo miti yote ya shambani ikanyauka. 16Niliyafanya mataifa yatetemeke kwa kishindo cha kuanguka kwake wakati nilipoushusha chini kaburini pamoja na wale wanaoshuka shimoni. Ndipo miti yote ya Edeni, miti iliyo bora kuliko yote na iliyo mizuri sana ya Lebanoni, miti yote ile iliyokunywa maji vizuri, ilifarijika hapa duniani. 17Wale walioishi katika kivuli chake, wale walioungana naye miongoni mwa mataifa, nao pia walikuwa wamezikwa pamoja naye, wakiungana na wale waliouawa kwa upanga.
18“ ‘Ni miti ipi ya Edeni inayoweza kulinganishwa nawe kwa fahari na utukufu? Hata hivyo, wewe pia, utashushwa pamoja na miti ya Edeni hadi chini kabisa; utalala miongoni mwa wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga.
“ ‘Huyu ni Farao pamoja na makundi yake yote, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
Iliyochaguliwa sasa
Ezekieli 31: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.