Ezekieli 33:1-9
Ezekieli 33:1-9 NENO
Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: “Mwanadamu, sema na watu wako uwaambie, ‘Nitakapoleta upanga dhidi ya nchi, nao watu wa nchi wakamchagua mmoja wa watu wao na kumfanya awe mlinzi wao, naye auonapo upanga unakuja dhidi ya nchi na kupiga tarumbeta kuonya watu, kama mtu yeyote asikiapo sauti ya tarumbeta hatakubali kuonywa, basi upanga ujapo na kuutoa uhai wake, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe. Kwa kuwa alisikia sauti ya tarumbeta lakini hakukubali maonyo, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe. Kama angekubali maonyo, angejiokoa mwenyewe. Lakini kama mlinzi akiona upanga unakuja na asipige tarumbeta kuonya watu na upanga ukija na kutoa uhai wa mmoja wao, yule mtu ataondolewa kwa sababu ya dhambi yake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwa mlinzi huyo.’ “Mwanadamu, nimekufanya wewe kuwa mlinzi kwa ajili ya nyumba ya Israeli, kwa hiyo sikia neno nisemalo na uwape maonyo kutoka kwangu. Nimwambiapo mtu mwovu, ‘Ewe mtu mwovu, hakika utakufa,’ nawe hukusema neno la kumwonya ili atoke katika njia zake, yule mtu mwovu atakufa kwa ajili ya dhambi yake, lakini mimi nitaitaka damu yake mkononi mwako. Lakini kama utamwonya huyo mtu mwovu aache njia zake mbaya naye hafanyi hivyo, atakufa kwa ajili ya dhambi yake, lakini utakuwa umejiokoa mwenyewe.