Ezekieli 33
33
Kuimarishwa kwa wajibu wa Ezekieli
1Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 2“Mwanadamu, sema na watu wako uwaambie, ‘Nitakapoleta upanga dhidi ya nchi, nao watu wa nchi wakamchagua mmoja wa watu wao na kumfanya awe mlinzi wao, 3naye auonapo upanga unakuja dhidi ya nchi na kupiga tarumbeta kuonya watu, 4kama mtu yeyote asikiapo sauti ya tarumbeta hatakubali kuonywa, basi upanga ujapo na kuutoa uhai wake, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe. 5Kwa kuwa alisikia sauti ya tarumbeta lakini hakukubali maonyo, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe. Kama angekubali maonyo, angejiokoa mwenyewe. 6Lakini kama mlinzi akiona upanga unakuja na asipige tarumbeta kuonya watu na upanga ukija na kutoa uhai wa mmoja wao, yule mtu ataondolewa kwa sababu ya dhambi yake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwa mlinzi huyo.’
7“Mwanadamu, nimekufanya wewe kuwa mlinzi kwa ajili ya nyumba ya Israeli, kwa hiyo sikia neno nisemalo na uwape maonyo kutoka kwangu. 8Nimwambiapo mtu mwovu, ‘Ewe mtu mwovu, hakika utakufa,’ nawe hukusema neno la kumwonya ili atoke katika njia zake, yule mtu mwovu atakufa kwa ajili ya dhambi yake, lakini mimi nitaitaka damu yake mkononi mwako. 9Lakini kama utamwonya huyo mtu mwovu aache njia zake mbaya naye hafanyi hivyo, atakufa kwa ajili ya dhambi yake, lakini utakuwa umejiokoa mwenyewe.
10“Mwanadamu, sema na nyumba ya Israeli uwaambie, ‘Hili ndilo mnalosema: “Makosa yetu na dhambi zetu zimetulemea, nasi tunadhoofika kwa sababu ya hayo. Tutawezaje basi kuishi?” ’ 11Waambie, ‘Hakika kama mimi niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, sifurahii kifo cha watu waovu, bali kwamba wageuke kutoka njia zao mbaya wapate kuishi. Geukeni! Geukeni kutoka njia zenu mbaya! Kwa nini mkafe, ee nyumba ya Israeli?’
12“Kwa hiyo, mwanadamu, waambie watu wako, ‘Haki ya mtu mwenye haki haitamwokoa wakati anapoacha kutii, wala uovu wa mtu mwovu hautamsababisha yeye kuanguka anapotubu na kuacha uovu. Mtu mwenye haki akitenda dhambi, hataishi kwa sababu ya uadilifu wake wa awali.’ 13Nikimwambia mtu mwenye haki kwamba hakika ataishi, lakini akategemea hiyo haki yake na kutenda uovu, hakuna tendo lolote la haki alilotenda litakalokumbukwa; atakufa kwa ajili ya uovu alioutenda. 14Nami nikimwambia mtu mwovu, ‘Hakika utakufa,’ kisha akageuka kutoka dhambi yake na kufanya lile lililo haki na sawa, 15kama akirudisha kile alichochukua rehani kwa ajili ya deni, akarudisha alichoiba na kufuata amri zile ziletazo uzima, wala hafanyi uovu, hakika ataishi, hatakufa. 16Hakuna dhambi yoyote aliyoitenda itakayokumbukwa juu yake. Ametenda lile lililo haki na sawa, hakika ataishi.
17“Lakini watu wako wanasema, ‘Njia ya Bwana si sawa.’ Lakini ni njia zao ambazo si sawa. 18Kama mtu mwenye haki akigeuka kutoka uadilifu wake na kufanya uovu, atakufa kwa ajili ya huo uovu. 19Naye mtu mwovu akigeuka kutoka uovu wake na kufanya lile lililo haki na sawa, kwa kufanya hivyo ataishi. 20Lakini, ee nyumba ya Israeli, unasema, ‘Njia ya Bwana si sawa.’ Lakini nitamhukumu kila mmoja wenu sawasawa na njia zake mwenyewe.”
Kuelezea kuanguka kwa Yerusalemu
21Mwaka wa kumi na mbili wa uhamisho wetu, mwezi wa kumi, siku ya tano, mtu aliyekuwa ametoroka kutoka Yerusalemu akanijia na kusema, “Mji wa Yerusalemu umeanguka!” 22Basi jioni kabla mtu huyo hajaja, mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa juu yangu, naye alifungua kinywa changu kabla ya mtu yule aliyenijia asubuhi hajafika. Basi kinywa changu kilifunguliwa na sikuweza tena kunyamaza.
23Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 24“Mwanadamu, watu wanaoishi katika magofu hayo katika nchi ya Israeli wanasema hivi, ‘Ibrahimu alikuwa mtu mmoja tu, hata hivyo akaimiliki nchi. Lakini sisi ni wengi, hakika tumepewa nchi kuwa milki yetu.’ 25Kwa hiyo waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa kuwa mnakula nyama ikiwa na damu, na kuinulia sanamu zenu macho na kumwaga damu, je, mtaimiliki nchi? 26Mnategemea panga zenu, mnafanya mambo ya machukizo na kila mmoja wenu humnajisi mke wa jirani yake. Je, mtaimiliki nchi?’
27“Waambie hivi: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Hakika kama niishivyo, wale waliobaki katika magofu wataanguka kwa upanga, wale walio nje mashambani nitawatoa wararuliwe na wanyama pori, nao wale walio katika ngome na kwenye mapango watakufa kwa tauni. 28Nitaifanya nchi ukiwa, na kiburi cha nguvu zake kitafikia mwisho, nayo milima ya Israeli itakuwa ukiwa ili mtu yeyote asipite huko. 29Kisha watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapokuwa nimeifanya nchi ukiwa kwa sababu ya mambo yote ya machukizo waliyotenda.’
30“Kwako wewe, mwanadamu, watu wako wanaongea habari zako wakiwa karibu na kuta na kwenye milango ya nyumba, wakiambiana kila mmoja na mwenzake, ‘Njooni msikie ujumbe ule unaotoka kwa Mwenyezi Mungu.’ 31Watu wangu wanakujia, kama wafanyavyo, nao wanaketi mbele yako kama watu wangu na kusikiliza maneno yako, lakini hawayatendi. Kwa maana udanganyifu u katika midomo yao, lakini mioyo yao ina tamaa ya faida isiyo halali. 32Naam, mbele yao umekuwa tu kama yeye aimbaye nyimbo za mapenzi kwa sauti nzuri za kuvutia na kupiga vyombo kwa ustadi, kwa kuwa wanasikia maneno yako lakini hawayatendi.
33“Mambo haya yote yatakapotimia, kwa kuwa hakika yatatokea, ndipo watajua kuwa nabii amekuwa miongoni mwao.”
Iliyochaguliwa sasa
Ezekieli 33: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.