Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 34

34
Mwenyezi Mungu atakuwa mchungaji wa Israeli
1Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 2“Mwanadamu, tabiri dhidi ya wachungaji wa Israeli, tabiri na uwaambie: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ole kwa wachungaji wa Israeli ambao hujitunza wenyewe tu! Je, haiwapasi wachungaji kutunza kundi la kondoo? 3Mnakula mafuta ya wanyama, mnavaa mavazi ya sufu na kuchinja kondoo walionona, lakini hamlitunzi kundi. 4Hamkuwatia nguvu walio dhaifu, wala kuwaganga wenye maradhi, wala kuwafunga waliojeruhiwa. Hamkuwarudisha waliotangatanga wala kuwatafuta wale waliopotea. Badala yake mmewatawala kwa ukali na kwa ukatili. 5Hivyo walitawanyika kwa sababu hapakuwa na mchungaji, nao walipotawanyika, wakawa chakula cha wanyama mwitu wote. 6Kondoo wangu walitangatanga kwenye milima yote na kwenye kila kilima kirefu. Kondoo wangu walitawanyika duniani kote, bila yeyote wa kuwaulizia wala kuwatafuta.
7“ ‘Kwa hiyo, ninyi wachungaji, lisikieni neno la Mwenyezi Mungu: 8Kwa hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, kwa sababu kondoo wangu wamekosa mchungaji na hivyo wametekwa nyara na kuwa chakula cha wanyama pori wote na kwa sababu wachungaji wangu, hawakuwatafuta kondoo wangu, bali wachungaji wamejitunza wenyewe, nao hawakuwalisha kondoo wangu, 9kwa hiyo enyi wachungaji, sikieni neno la Mwenyezi Mungu: 10Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mimi ni kinyume na wachungaji, nami nitawadai kondoo wangu mikononi mwao. Nitawafukuza kutoka kuchunga kundi langu, ili wachungaji wasiendelee kujitunza wenyewe. Nitaokoa kondoo wangu kutoka vinywa vyao, nao kondoo hawatakuwa tena chakula chao.
11“ ‘Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mimi mwenyewe nitawaulizia kondoo wangu na kuwatafuta. 12Kama vile mchungaji atafutavyo kundi lake lililotawanyika wakati akiwa pamoja nalo, hivyo ndivyo nitakavyowatafuta kondoo wangu. Nitawaokoa kutoka mahali pote walipokuwa wametawanyikia katika siku ya mawingu na giza nene. 13Nitawatoa katika mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mbalimbali, nami nitawaleta katika nchi yao wenyewe. Nitawalisha kwenye milima ya Israeli, katika mabonde na pia mahali pote panapokaliwa katika nchi. 14Nitawachunga kwenye malisho mazuri na miinuko ya mlima wa Israeli patakuwa mahali pao pa malisho. Huko watajipumzisha katika nchi ya malisho mazuri, nao watajilisha huko katika malisho tele katika milima ya Israeli. 15Mimi mwenyewe nitawachunga kondoo wangu na kuwafanya wapumzike, asema Bwana Mungu Mwenyezi. 16Nitawaulizia kondoo waliopotea na kuwaleta waliotangatanga. Nitawafunga waliojeruhiwa na kuwatia nguvu walio dhaifu, lakini wale walionona na wenye nguvu nitawaangamiza. Nitalichunga kundi kwa haki.
17“ ‘Kwenu ninyi, kundi langu, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitahukumu kati ya kondoo na kondoo, kati ya kondoo dume na mbuzi. 18Je, haiwatoshi ninyi kujilisha kwenye malisho mazuri? Je, ni lazima ninyi kuyakanyaga pia malisho yenu yaliyobaki kwa miguu yenu? Je, haiwatoshi ninyi kunywa maji safi? Je, ni lazima kuyachafua maji mengine kwa miguu yenu? 19Je, ni lazima kundi langu wajilishe kwa yale mliyoyakanyaga na kunywa maji mliyoyachafua kwa miguu yenu?
20“ ‘Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mungu Mwenyezi awaambialo: Tazama, mimi mwenyewe nitahukumu kati ya kondoo wanono na waliokonda. 21Kwa sababu mmewapiga kikumbo na kuwapiga kwa pembe zenu kondoo wote walio dhaifu hadi wakawafukuza, 22nitaliokoa kundi langu na hawatatekwa nyara tena. Nitahukumu kati ya kondoo na kondoo. 23Nitaweka juu yao mchungaji mmoja, mtumishi wangu Daudi, naye atawachunga, atawachunga na kuwa mchungaji wao. 24Mimi Mwenyezi Mungu nitakuwa Mungu wao, naye mtumishi wangu Daudi atakuwa mkuu miongoni mwao. Mimi Mwenyezi Mungu nimenena.
25“ ‘Nitafanya nao agano la amani na kuwaondoa wanyama mwitu kutoka nchi yao ili kondoo wangu waweze kupumzika nyikani na msituni kwa salama. 26Nitawabariki wao pamoja na maeneo yanayozunguka kilima changu. Nitawanyeshea mvua kwa majira yake, kutakuwa na mvua za baraka. 27Miti ya shambani itatoa matunda yake na ardhi itatoa mazao yake, watu watakaa salama katika nchi yao. Watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapovunja vifungo vya nira zao na kuwaokoa kutoka mikono ya wale waliowafanya watumwa. 28Hawatatekwa tena nyara na mataifa, wala wanyama pori kuwala tena. Wataishi kwa salama, wala hakuna yeyote atakayewatia hofu. 29Nitawapa nchi yenye sifa kutokana na mazao yake, na hawatapatwa na njaa katika nchi tena, wala kudharauliwa na mataifa. 30Ndipo watajua kuwa Mimi, Mwenyezi Mungu, Mungu wao, niko pamoja nao, na kwamba wao, nyumba ya Israeli, ni watu wangu, asema Bwana Mungu Mwenyezi. 31Ninyi ni kondoo wangu, kondoo wa malisho yangu; ninyi ni watu wangu, nami ni Mungu wenu, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”

Iliyochaguliwa sasa

Ezekieli 34: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia