Ezekieli 46:16-24
Ezekieli 46:16-24 NEN
“ ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ikiwa mkuu atawalaye atatoa zawadi kutoka kwenye urithi wake na kumpa mmoja wa wanawe, hiyo zawadi itakuwa pia kwa wazao wake, itakuwa mali yao kwa urithi. Hata hivyo, kama atatoa zawadi kutoka urithi wake na kumpa mmoja wa watumishi wake, mtumishi anaweza kuiweka mpaka mwaka wa uhuru, kisha itarudishwa kwa mkuu anayetawala. Urithi wake ni wa wanawe peke yao, ni mali yao. Mkuu anayetawala hana ruhusa kuchukua urithi wowote wa watu na kuwaondoa kwenye mali zao. Mkuu atawalaye atawapa wanawe urithi wao, kutoka kwenye mali zake mwenyewe, ili kwamba pasiwe na mtu wangu yeyote atakayetengwa na urithi wake.’ ” Kisha mtu yule akanileta kwa kupitia kwenye ingilio lililokuwa kando ya lango mpaka kwenye vyumba vitakatifu vinavyoelekea kaskazini, ambavyo ni vya makuhani, naye akanionyesha mahali fulani upande wa mwisho wa magharibi. Akaniambia, “Mahali hapa ndipo makuhani watakapotokosea sadaka ya hatia na sadaka ya dhambi na kuoka sadaka ya nafaka, kuepuka kuzileta katika ukumbi wa nje na kushirikisha utakatifu kwa watu.” Baada ya hapo akanileta kwenye ukumbi wa nje na kunizungusha kwenye pembe zake nne, nami nikaona katika kila pembe ya huo ukumbi kulikuwa na ukumbi mwingine. Katika pembe nne za huo ukumbi wa nje kulikuwa na kumbi nyingine, zenye urefu wa dhiraa arobaini na upana wake dhiraa thelathini, ambapo hizo kumbi kwenye hizo pembe nne zilikuwa na vipimo vilivyo sawa. Mzunguko wa ndani wa hizo kumbi nne ulikuwa na ukingo wa jiwe, zikiwa na sehemu zilizojengwa kwa ajili ya moto kuzunguka chini ya huo ukingo. Akaniambia, “Hizi ndizo sehemu za kupikia ambazo wale wanaohudumu kwenye Hekalu watatokosea dhabihu za watu.”