Wagalatia 4:19-31
Wagalatia 4:19-31 NENO
Watoto wangu wapendwa, ambao kwa mara nyingine ninawaonea uchungu, ninatamani kwamba Al-Masihi aumbike ndani yenu. Natamani kama ningekuwa pamoja nanyi sasa, pengine ningebadilisha sauti yangu. Kwa maana nina wasiwasi kwa ajili yenu. Niambieni, ninyi mnaotaka kuwa chini ya sheria, je, hamjui sheria inavyosema? Kwa maana imeandikwa kwamba Ibrahimu alikuwa na wana wawili, mmoja wa mwanamke mtumwa na wa pili wa mwanamke huru. Lakini, mtoto wa mwanamke mtumwa alizaliwa kwa mapenzi ya mwili, na yule mwingine wa mwanamke huru alizaliwa kutokana na ahadi ya Mungu. Mambo haya yanaweza kuchukuliwa kama mfano. Kwa maana hao wanawake wawili ni mfano wa maagano mawili: Agano la kwanza ni lile lililofanyika katika Mlima Sinai, linalozaa watoto wa utumwa. Hili ndilo huyo Hajiri. Basi Hajiri anawakilisha Mlima Sinai ulio Arabuni, na unafanana na Yerusalemu ya sasa ambayo iko utumwani pamoja na watoto wake. Lakini Yerusalemu wa juu ni huru, nayo ndiye mama yetu. Kwa maana imeandikwa: “Furahi, ewe mwanamke tasa, wewe usiyezaa; paza sauti, na kuimba kwa furaha, wewe usiyepatwa na uchungu wa kuzaa; kwa maana watoto wa mwanamke aliyeachwa ukiwa ni wengi kuliko wa mwanamke mwenye mume.” Basi, sisi ndugu zangu, ni kama Isaka, tu watoto wa ahadi. Lakini, kama vile ilivyokuwa siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomchokoza yule aliyezaliwa kwa uweza wa Roho wa Mungu, ndivyo ilivyo hata sasa. Lakini Maandiko yasemaje? “Mwondoe mwanamke mtumwa pamoja na mwanawe, kwa sababu mwana wa mwanamke mtumwa kamwe hatarithi pamoja na mwana wa aliye huru.” Kwa hiyo ndugu zangu, sisi si watoto wa mwanamke mtumwa, bali wa yule aliye huru.