Wagalatia 4
4
1Lile nisemalo ni kwamba wakati wote mrithi bado ni mtoto, hana tofauti na mtumwa, ingawa ndiye mmiliki wa mali yote. 2Yeye huwa chini ya uangalizi wa walezi na wadhamini hadi ufike wakati uliowekwa na baba yake. 3Vivyo hivyo na sisi, tulipokuwa bado watoto wadogo, tulikuwa utumwani chini ya taratibu za kawaida za ulimwengu. 4Lakini wakati uliopangwa ulipotimia, Mungu alimtuma Mwanawe, ambaye alizaliwa na mwanamke, akazaliwa chini ya sheria, 5ili awakomboe wale waliokuwa chini ya sheria, nasi tupate kupokea zile haki kamili za kufanywa wana. 6Kwa sababu ninyi ni watoto wa Mungu, Mungu amemtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, anayelia, “Abba#4:6 Abba ni neno la Kiaramu ambalo maana yake ni Baba., Baba.” 7Kwa hiyo, wewe si mtumwa tena, bali ni mwana. Na kwa kuwa wewe ni mwana, Mungu amekufanya wewe pia kuwa mrithi kupitia kwa Al-Masihi.
Paulo awashawishi Wagalatia
8Zamani, mlipokuwa hammjui Mungu, mlikuwa watumwa wa viumbe ambavyo kwa asili si Mungu. 9Lakini sasa kwa kuwa mmemjua Mungu, au zaidi mmejulikana na Mungu, inakuwaje mnarejea tena katika zile kanuni za kwanza zenye udhaifu na upungufu? Mnataka ziwafanye tena watumwa? 10Mnaadhimisha siku maalum, miezi, nyakati na miaka! 11Nina hofu juu yenu, kwamba kazi niliyofanya kwa ajili yenu inaweza kuwa nimejitaabisha bure.
12Ndugu zangu, nawasihi mwe kama mimi, kwa sababu mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunitendea jambo lolote baya. 13Ninyi mwajua kwamba ni kwa ajili ya udhaifu wangu niliwahubiria Injili. 14Ingawa hali yangu iliwatia majaribuni, hamkunidharau wala kunidhihaki, bali mlinikaribisha kama malaika wa Mungu, kama vile Al-Masihi Isa. 15Ile hali ya furaha mliyokuwa nayo imeenda wapi? Naweza kushuhudia kwamba, kama ingewezekana mngeng’oa macho yenu na kunipa mimi. 16Je, sasa nimekuwa adui yenu kwa kuwaambia ukweli?
17Hao wana shauku ya kuwapata lakini si kwa kusudi zuri. Wanachotaka ni kuwatenga mbali nasi, ili ninyi mpate kuwaonea wao shauku. 18Ni vizuri wakati wote kuwa na shauku kwa ajili ya kusudi zuri, si wakati nikiwa pamoja nanyi tu. 19Watoto wangu wapendwa, ambao kwa mara nyingine ninawaonea uchungu, ninatamani kwamba Al-Masihi aumbike ndani yenu. 20Natamani kama ningekuwa pamoja nanyi sasa, pengine ningebadilisha sauti yangu. Kwa maana nina wasiwasi kwa ajili yenu.
Mfano wa Hajiri na Sara
21Niambieni, ninyi mnaotaka kuwa chini ya sheria, je, hamjui sheria inavyosema? 22Kwa maana imeandikwa kwamba Ibrahimu alikuwa na wana wawili, mmoja wa mwanamke mtumwa na wa pili wa mwanamke huru. 23Lakini, mtoto wa mwanamke mtumwa alizaliwa kwa mapenzi ya mwili, na yule mwingine wa mwanamke huru alizaliwa kutokana na ahadi ya Mungu.
24Mambo haya yanaweza kuchukuliwa kama mfano. Kwa maana hao wanawake wawili ni mfano wa maagano mawili: Agano la kwanza ni lile lililofanyika katika Mlima Sinai, linalozaa watoto wa utumwa. Hili ndilo huyo Hajiri. 25Basi Hajiri anawakilisha Mlima Sinai ulio Arabuni, na unafanana na Yerusalemu ya sasa ambayo iko utumwani pamoja na watoto wake. 26Lakini Yerusalemu wa juu ni huru, nayo ndiye mama yetu. 27Kwa maana imeandikwa:
“Furahi, ewe mwanamke tasa,
wewe usiyezaa;
paza sauti, na kuimba kwa furaha,
wewe usiyepatwa na uchungu wa kuzaa;
kwa maana watoto wa mwanamke aliyeachwa ukiwa ni wengi
kuliko wa mwanamke mwenye mume.”#4:27 Isaya 54:1
28Basi, sisi ndugu zangu, ni kama Isaka, tu watoto wa ahadi. 29Lakini, kama vile ilivyokuwa siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomchokoza yule aliyezaliwa kwa uweza wa Roho wa Mungu, ndivyo ilivyo hata sasa. 30Lakini Maandiko yasemaje? “Mwondoe mwanamke mtumwa pamoja na mwanawe, kwa sababu mwana wa mwanamke mtumwa kamwe hatarithi pamoja na mwana wa aliye huru.”#4:30 Mwanzo 21:10 31Kwa hiyo ndugu zangu, sisi si watoto wa mwanamke mtumwa, bali wa yule aliye huru.
Iliyochaguliwa sasa
Wagalatia 4: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.