Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wagalatia 3

3
Imani na Torati
1Ninyi Wagalatia wajinga! Ni nani aliyewaroga? Isa Al-Masihi aliwekwa wazi mbele yenu kwamba amesulubiwa. 2Nataka nijifunze neno moja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa kushika Torati, au kwa kuyaamini yale mliyosikia? 3Je, ninyi ni wajinga kiasi hicho? Baada ya kuanza kwa Roho, je, sasa mwataka kumalizia katika mwili? 4Je, mlipata mateso kiasi hicho bure? Ni kama kweli yalikuwa bure! 5Je, Mungu huwapa Roho wake Mtakatifu na kufanya miujiza kati yenu kwa sababu mnatii Torati, au kwa sababu mnaamini kile mlichosikia? 6Kama vile “Ibrahimu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”#3:6 Mwanzo 15:6
7Fahamuni basi kwamba wale walio na imani, hao ndio watoto wa Ibrahimu. 8Andiko liliona tangu awali kwamba Mungu angewahesabia haki watu wa Mataifa kwa imani, hivyo likatangulia kumtangazia Ibrahimu Injili, likisema kwamba, “Kupitia kwako mataifa yote yatabarikiwa.”#3:8 Mwanzo 12:3; 18:18; 22:18 9Kwa sababu hii, wale wote wanaoamini wanabarikiwa pamoja na Ibrahimu, mtu wa imani.
Torati na laana
10Kwa maana wote wanaotumainia matendo ya Torati wako chini ya laana, kwa kuwa imeandikwa, “Alaaniwe kila mtu asiyeshikilia kutii mambo yote yaliyoandikwa katika Kitabu cha Torati.”#3:10 Kumbukumbu 27:26 11Basi ni dhahiri kwamba hakuna mtu anayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kushikilia Torati, kwa maana, “Mwenye haki ataishi kwa imani.”#3:11 Habakuki 2:4 12Lakini Torati haitegemei imani. Kinyume chake, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.”#3:12 Walawi 18:5 13Al-Masihi alitukomboa kutoka laana ya Torati kwa kufanyika laana kwa ajili yetu, kwa maana imeandikwa, “Amelaaniwa yeye aangikwaye juu ya mti.”#3:13 Kumbukumbu 21:23 14Alitukomboa ili baraka aliyopewa Ibrahimu ipate kuwafikia watu wa Mataifa kupitia kwa Al-Masihi Isa, ili kwa imani tupate kupokea ile ahadi ya Roho wa Mungu.
Torati na ahadi
15Ndugu zangu, nataka nitoe mfano kutoka maisha ya kila siku. Kama vile hakuna mtu awezaye kutangua au kuongeza kitu katika agano la mtu ambalo limekwisha kuthibitishwa, vivyo hivyo kwa hali kama hii. 16Ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Maandiko hayasemi “kwa uzao”#3:16 Mwanzo 12:7; 13:15; 24:7, yakimaanisha watu wengi, bali “kwa mzao wako”, yaani mtu mmoja, ndiye Al-Masihi. 17Ninachotaka kusema ni kwamba, Torati, ambayo ilitolewa miaka mia nne na thelathini (430) baadaye, haitangui agano lililothibitishwa na Mungu ili kuibatilisha ahadi ile. 18Kwa maana kama urithi hupatikana kwa Torati, basi hautegemei tena ahadi, lakini Mungu kwa neema yake alimpa Ibrahimu urithi kupitia kwa ahadi.
Kusudi la Torati
19Kwa nini basi iwepo Torati? Torati iliwekwa kwa sababu ya makosa hadi atakapokuja yule Mzao wa Ibrahimu, ambaye alitajwa katika ile ahadi. Torati iliamriwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi. 20Basi mpatanishi huhusisha zaidi ya upande mmoja, lakini Mungu ni mmoja.
21Je basi, Torati inapingana na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa maana kama Torati iliyotolewa ingeweza kuwapa watu uzima, basi haki ingepatikana kupitia kwa Torati. 22Lakini Maandiko yamefanya vitu vyote vifungwe chini ya nguvu ya dhambi, ili yale yaliyoahidiwa kupitia kwa imani katika Isa Al-Masihi yapate kupewa wale wanaoamini.
23Kabla imani hii haijaja tulikuwa tumewekwa chini ya Torati, tumefungwa hadi ile imani ifunuliwe. 24Hivyo, Torati ilikuwa kiongozi kutufikisha kwa Al-Masihi, ili tupate kuhesabiwa haki kwa imani. 25Lakini sasa kwa kuwa ile imani imekuja, hatusimamiwi tena na Torati.
Watoto wa Mwenyezi Mungu
26Kwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Al-Masihi Isa kupitia kwa imani. 27Kwa maana wote mliobatizwa#3:27 Ubatizo ni ishara ya kuungama dhambi na kusamehewa na Mwenyezi Mungu, na kuweka nadhiri ya kubadilisha mienendo ya awali. Wafuasi wa Isa Al-Masihi pia wanapokea Roho wa Mungu kama dhibitisho ya imani yao. ndani ya Al-Masihi, mmemvaa Al-Masihi. 28Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Al-Masihi Isa. 29Nanyi mkiwa ni mali ya Al-Masihi, basi ninyi ni wa uzao wa Ibrahimu na warithi sawasawa na ile ahadi.

Iliyochaguliwa sasa

Wagalatia 3: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia