Wagalatia 4:8-18
Wagalatia 4:8-18 NENO
Zamani, mlipokuwa hammjui Mungu, mlikuwa watumwa wa viumbe ambavyo kwa asili si Mungu. Lakini sasa kwa kuwa mmemjua Mungu, au zaidi mmejulikana na Mungu, inakuwaje mnarejea tena katika zile kanuni za kwanza zenye udhaifu na upungufu? Mnataka ziwafanye tena watumwa? Mnaadhimisha siku maalum, miezi, nyakati na miaka! Nina hofu juu yenu, kwamba kazi niliyofanya kwa ajili yenu inaweza kuwa nimejitaabisha bure. Ndugu zangu, nawasihi mwe kama mimi, kwa sababu mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunitendea jambo lolote baya. Ninyi mwajua kwamba ni kwa ajili ya udhaifu wangu niliwahubiria Injili. Ingawa hali yangu iliwatia majaribuni, hamkunidharau wala kunidhihaki, bali mlinikaribisha kama malaika wa Mungu, kama vile Al-Masihi Isa. Ile hali ya furaha mliyokuwa nayo imeenda wapi? Naweza kushuhudia kwamba, kama ingewezekana mngeng’oa macho yenu na kunipa mimi. Je, sasa nimekuwa adui yenu kwa kuwaambia ukweli? Hao wana shauku ya kuwapata lakini si kwa kusudi zuri. Wanachotaka ni kuwatenga mbali nasi, ili ninyi mpate kuwaonea wao shauku. Ni vizuri wakati wote kuwa na shauku kwa ajili ya kusudi zuri, si wakati nikiwa pamoja nanyi tu.